Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza zimebainisha kuwa tukio hilo limetokea saa 9.30 alasiri wakati askari hao wakiwa katika doria baada ya boti yao aina ya Fibre kupigwa na mawimbi mazito na kupinduka.
Akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Nonosius Komba amemtaja aliyekufa kuwa ni Lensikoplo Majaliwa Shabaan Kagoma (47) aliyekuwa kiongozi wa doria.
Amewataja walionusurika kuwa ni Julius Indaya (37) na Francis Maseku (27) ambao wanadiwa baada ya kupinduka waliendelea kuushikilia mtumbwi kwa juu na kuogelea wakiusukuma mpaka nchi kavu na hivyo kunusurika.
Hata hivyo, Lensikoplo Majaliwa anadaiwa kuwa yeye alizama moja kwa moja akiwa na bunduki ameivaa na kasha la kuhifadhia risasi (magazine) ikiwa na risasi 30 ambapo zoezi kali kwa kushirikisha wadau mbalimbali la uokoaji linaendelea.
Hili ni tukio la pili kutokea katika eneo hilo hilo la Ilumo kisiwani humo, ambapo mwaka juzi pia askari mwingine wa hifadhi hiyo alikufa maji akiwa na bunduki aina ya SMG na risasi katika mazingira yaliyodaiwa huenda katika kurupukushani ya kukabiliana na wavuvi haramu wakiwepo katika doria.
Wakati huo huo jeshi la polisi wilayani Geita limemfikisha mahakamani katika mahakama ya wilaya, mtuhumiwa Samweli Matiku (50), mfanyabiashara wa maduka ya nyama, mkazi wa kijiji cha Nyamarembo mjini Geita kwa tuhuma za wizi wa mifugo.
Mtuhumiwa baada ya kusomewa mashtaka aliachiwa kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena wiki ijayo ambapo inadaiwa kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana lakini mwenyewe anakana kuhusika.
0 Comments