Waziri mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi ameonekana kwenye televisheni ya taifa kutangaza kuwa Rais Ben Ali amemkabidhi madaraka kwa muda.
Bw Ghannouchi alisema Rais Ben Ali hakuweza kutimiza wajibu wake kwa muda.Kwa sasa haijulikani Rais Ben Ali alipo.
Hali ya hatari imetangazwa nchini Tunisia huku maandamano yakiendelea kuhusu ukosefu wa ajira na mfumko wa bei.
Kwa sasa hairuhusiwi zaidi ya watu watatu kukutana hadharani.
Wakati huo huo Rais Zine al-Abidine Ben Ali amevunja serikali yake na kutangaza uchaguzi kufanyika katika kipindi cha miezi sita.
Maelfu ya watu wamekusanyika kwenye mji mkuu wa Tunis wakimtaka rais kujiuzulu.
Alhamisi usiku, Ben Ali, ambaye ameiongoza Tunisia tangu 1987, alitangaza kuondoka madarakani mwaka wa 2014 - lakini waandamanaji wanataka aondoke sasa.
Polisi waliwafyatulia mabomu ya machozi waandamanaji nje ya wizara ya mambo ya ndani.
Madaktari wamethibitisha kuwa watu 13 waliuawa wakati wa makabiliano usiku kwenye mji mkuu na kuna taarifa zinazosema kuwa watu watano wameuawa katika maandamano ya siku ya Ijumaa.
Makundi ya kutetea haki za binadamu wanasema zaidi ya watu 60 wameuawa kwenye ghasia tangu zianze.
0 Comments