Serikali imesema maji ya kunywa yanayozalishwa na kampuni 47 nchini, yanakidhi ubora wa viwango.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Charles Ekelege, alipokuwa akielezea changamoto mbalimbali za ubora wa maji ya kunywa yalifofungashwa.
Alisema maji ya kunywa yaliyofungashwa ya chupa yaliyothibitishwa ubora wake na yaliyowekewa alama ya ubora ya TBS ni salama kunywa.
“Shirika linadhibiti ili kuhakikisha kuwa matakwa yote yaliyo kwenye kiwango husika yanafikiwa kabla maji husika ya kunywa hayajapata cheti cha TBS,” alisema.
Ekelege aliongeza kuwa maofisa wa TBS wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara viwandani na katika soko,
Alisema lengo la ukaguzi wa kushtukiza ni kuhakikisha kuwa wazalishaji wa maji ya chupa ya kunywa wanaendelea kuzalisha maji yenye ubora.
Ili kuhakikishia umma kuwa shughuli za TBS zinatambulika kimataifa, TBS imepata uthibitisho kutoka katika vyombo huru.
“TBS inapenda kusisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria ya viwango namba 2 ya mwaka 2009 ina mamlaka ya kudhibiti ubora wa maji ya kunywa,” alisema.
Awali ilidaiwa kuwa maji mengi ya kunywa yanayouzwa maeneo mbali mbali yamekuwa si salama kwa afya ya binadamu kutokana na kutokuwa na kiwango kinachotakiwa.
Akizungumza katika mhadhara wa kiprofesa uliofanyika hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete, alisema maji mengi ya chupa sio salama kwa kuwa ubora wake unatia mashaka.
Profesa Mbwete ambaye ni mtaalam wa Sayansi ya Mazingira na Teknolojia, alikuwa anawasilisha mada kuhusu usalama wa maji ya kunywa hasa yale ya chupa na athari za kuongezeka kwa wafanyabiashara wa maji hayo.
Alisema hali hiyo inachangiwa na baadhi ya chupa za maji hayo kutokuwa na tarehe inayoonyesha kumalizika kwa muda wa matumizi yake na mengine kukosa maelezo muhimu kwa watumiaji.
Alibainisha kuwa TBS ikishatoa kibali cha maji hayo kutumika, haina utaratibu wa kukagua maji yanayozalishwa na hivyo kuwapa wafanyabiashara nafasi ya kuweka katika chupa hizo maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu.
0 Comments