KABLA ya hotuba ya mwisho wa mwaka jana, ambapo Rais Jakaya Kikwete, pamoja na mambo mengine, alitangaza uamuzi wa kuanzisha mchakato wa kuunda Katiba mpya,
tulishuhudia mengi katika siasa.

Pengine washauri wa Rais Kikwete wanaona uundwaji wa tume ni suluhu ili kufikia malengo ya kupata katiba mpya. Hata hivyo siku chache kabla ya kutangazwa azma hiyo, tumeona namna baadhi ya wanasiasa na wananchi mbalimbali walivyoandamana kwa lengo la kudai katiba
mpya.
Kuandamana haigombi, ila tunapaswa kuangalia mwenendo mzima wa namna ya kuandamana. Hapo ndipo tafakuri huria inaanza kufanya kazi kwa maswali anuwai. Inaelekea siku hizi ili mtu athibitishe msimamo wake lazima akasirike, aanzishe vurumai na kupandisha
mori.

Siasa zetu siku hizi zimekuwa za kuchochea hasira na munkari usioeleweka mwanzo wake. Wenye dhamana ya kutuliza mori nao hupandisha mori, mitaani hakukaliki wala hakulaliki.

Siku hizi wenye kukunja nyuso zao kwa jazba ambazo huumba mistari mithili ya upinde wa mvua wanaelekea kuteka jamii, eti kwamba wajuvi wa kudai masuala ya msingi yenye maslahi kwa wananchi.

Wapo wanaodhani kuwa tabia za ubedui ndizo zinadhihirisha kwamba wao ni jogoo wanaojua kuliko wale waliokaa kimya au wanaofuata taratibu madhubuti kwa suala husika. Ugangwe ni mzuri kwa mwenye busara, lakini si kila kitu kinahitaji uwe gangwe ndiyo ueleweke.

Inawezekana ukawa mwehu kudai kitu mithili ya mwehu, lakini wehu huo una busara zake ambazo unakuondoa katika jopo la wehu halisi mitaani. Sote tunatambua Katiba ni mali yetu na ndiyo inayojenga msingi wa nchi yetu.

Tunajua kuwa kila Katiba inapohitaji marekebisho au kubadilishwa zipo taratibu za kufuatwa.
Taratibu zikifuatwa mambo yanakuwa kama tulivyoona Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amewasilisha hoja binafsi juu ya rasimu ya katiba mpya kwa katibu wa Bunge.

Mbunge Mnyika amefuata taratibu wala hajapandisha mori kuonesha ana hamu sana na katiba mpya. Hii ni busara na taratibu zinazopendeza watu wote. Na hamu yake inakuwa katika utaratibu wenye uchochezi kifikra kwakuwa tayari ameueleza katika njia halali.

Tunajua kuwa madai ya katiba mpya si mageni, wala hayataisha leo kwa kuwa jamii inabadilika
na kila mmoja anataka kujipendelea kwa lolote lililopo. Kila mmoja anatambua haki ya kuwa huru na kufanya mambo bila kuvunja Katiba.

Kila mmoja anaweza kushiriki siasa, lakini hakuna maana ushiriki huo uambatane na ngumi au
mateke. Kwamba kufanya hivyo ndio unadhihirisha umwamba wa madai yako juu ya Katiba. Dai haki yako kwa utaratibu unaoleweka.

Dai katiba mpya ukitofautisha na udai kitumbua cha chai ulichodhulumiwa nyumbani. Usijaribu kudai katika katiba mpya kama kudai bonasi kwa mwajiri wako unayejua mkorofi.
Kulinganisha madai ya katiba mpya na kudai andazi nyumbani ni mantiki iliyopinda.

Kudhani maguvu yanaweza kuzalisha katiba mpya mimi naamini tunakosa uelewa juu ya kusimamia madai. Usilinganishe kudai kalamu ya wino uliyoibiwa shule na suala la katiba
mpya.

Katiba mpya inahitaji watu wote waijadili, wachanganue, wahoji, wapime, waamue na kuikubali kuwa halali kutumika. Kama mkeo anavuruga bajeti ya nyumba basi panga njia
halali ya kudai mabadiliko, kumzaba ngumi na mateke haisaidii kitu.

Ni sawa na dai hili la katiba, tuidai katiba kwa adabu hata kama ni laiki yetu. Hili ni sawa suala linalojitokeza sasa kuwa kudai katiba mpya ni lazima watu kuanza kutoana ngeu. Huu ni ustaratibu wa kihuni, tunataka njia muafaka ya kuwasilisha madai yako.

Tumesikia wanachama wa Chama cha Wananchi (Cuf) wakilalamika kuzuiliwa na Jeshi la Polisi katika maandamano yao ya kuwasilisha rasimu ya katiba mpya. Wanachama wa Cuf walipandisha mori Buguruni na Ilala na kutishia kwenda kushitaki kwa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita iliyoko The Hague, Luis Moreno Ocampo.

Sote tunahitaji katiba mpya na tunaipenda nchi yetu, lakini tusichukue hatua ya kuipenda sana nchi yetu kuwa tiketi ya kufanya uhuni. Sidhani kama huyo Ocampo anaweza kuruhusu kupokea madai ya katiba mpya Tanzania kwa kutishwa kung’olewa meno.

Hatuhitaji ngumi wala mateke katika madai ya katiba mpya. Na kama ni ngumi iwe ile ya ngumi ya hoja ambao ikitua barabara kichwani inakuwia vigumu kupingana nayo. Watu wenye akili zao, na wenye kuelewa kabisa, na kwa moyo safi, wanaojua utaratibu wa kudai katiba
mpya wanaamua kuanzisha zogo la kutoana ngeu na kung’oana meno.

Hili si jambo zuri, maana tunajua kila zuri lina dosari zake. Nimebahatika kuisoma na kuzielewa katiba zote mbili yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Nakiri zipo dosari. Na dosari rahisi mno ilifanyika mwaka 1994 ya kuondoa kipengele cha makamu wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye alikuwa pia rais wa Zanzibar.
Kwa maoni yangu hatukupaswa kukiondoa kipengele hicho kwakuwa kinaonesha umuhimu mkubwa sana wa kuuthamini muungano wetu.

Kuondolewa kipengele hicho kinazorotesha muungano wetu na mshikamano uliopo. Pamoja na dosari hizo kujitokeza, lakini bado sijaona sababu ya kudai katiba mpya kwa msingi wa mangumi na mateke.

Wafuasi wa CUF wapoandamana kudai katiba, kwa mikogo mingi na harara inakithiri. Mikusanyiko na mijadala juu ya katiba mpya inafanyika kwa kutazamana usoni, kama hujashiriki katika kampeni ya kudai katiba kwa munkari basi unacharazwa mangumi na mateke.

Sijui huu ni utamaduni wa aina gani, na sijui kwamba ukiwa na hasira zako juu ya katiba mpya
ndiyo utaeleweka sana au la. Maandamano haya yamekuwa wakiwafanya polisi wawe makini na uendeshaji wake.

Suala la Katiba ni letu sote na linaihusu nchi yetu, lakini hakuna sababu ya msingi kutwangana
makonde na kuchaniana mashati kwa sababu ya kudai Katiba. Sote tunahitaji kujenga hekalu moja, hivyo basi tubomoe mlango huo kwa hekima.

Tunaruhusu Polisi kuvurumisha mabomu ili kutuliza jazba za waandamanaji wa kudai katiba mpya wakati hakuna sababu yoyote ya kudai katiba kwa mijeledi. Utamaduni wa kudai kila kitu
kwa mikwaruzano unashamiri, wapo wenye madai ya msingi lakini namna uwasilishaji wa vilio vyao na kwakutumia ngumi, mateke na mikwaju wanadhani wataeleweka.

Tusiige utamaduni wa ngumi na mateke kufanikisha azma zetu. Kati ya waandamanaji hawa ukiuliza anayejua hata Katiba hiyo wanayoikashifu, wengi hawana jawabu. Vuguvugu la kudai Katiba halimaanishi kwamba kila mtu akunje ngumi na kurusha kwa wengine au kulazimisha wengine washiriki madai haya.

Kila mmoja anapima kwa nafasi yake, anachanganua, anaafiki kuwa madai haya ni halali.
Na anayasimamia kwa uhalali wala havurumishi ngumi au teke kwa mdaiwa. Viongozi wasimamie hoja kwa utulivu, tuepuke tabia za amri.

Na Katiba yetu inakuja kwa namna tutakavyotaka. Amani iwe kwenu nyote.