Wachezaji nyota wanne wa Simba juzi usiku walimuweka kitimoto mwenyekiti wa klabu yao, Ismail Aden Rage wakimlalamikia kwamba mmoja wa viongozi wake wa juu anawagawa wachezaji.
Nyota hao (majina tunayahifadhi), juzi usiku walikaa na Rage kuanzia saa 3:05 hadi saa 3:40 wakimpa malalamiko yao katika hoteli ya nyota tatu waliyofikia ya Karthala iliyoko katika mji wa Mvuni, Kaskazini mwa Moroni.

Wachezaji hao walidai kuwa hali ndani ya timu yao si shwari kwa sababu wachezaji wamegawanyika na hiyo si ishara njema kwa timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na pia inayotetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Wachezaji hao waliiambia NIPASHE kuwa mbali na baadhi ya wenzao kuonekana ni bora na kupewa kipaumbele katika baadhi ya mambo, wanakerwa pia na tabia ya kuelezwa kuwa wanaihujumu timu pale inapopata matokeo mabaya katika mechi zao za ligi na za kirafiki.
Mchezaji mwingine alilalamika kwa Rage kuwa wanakerwa na kitendo cha kocha wao Patrick Phiri kuingiliwa katika maamuzi yake na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba.
Alisema imefikia wakati Phiri anashindwa kufanya maamuzi yake kama mtaalamu katika kupanga kikosi chake, jambo ambalo wanaona si zuri kwa mustakabali wa timu yao.
"Pale uwanjani (juzi) ilitukera sana wakati mmoja wao alipotoa lugha ya matusi, akimtaka Phiri afanye mabadiliko kwa sauti ya juu... wote tulisikia na jambo hili lilituumiza sana," alisema mchezaji mwingine.
Wachezaji hao walisema kuwa hali hiyo inapaswa kubadilika haraka ili timu ifanye vizuri na wachezaji wasiwe na kinyongo.
Kuhusiana na mechi hiyo, wachezaji hao walisema ilikuwa ngumu ila wana uwezo wa kuiondoa Elan katika mechi yao ya marudiano endapo jitihada za pamoja zitakuwepo.
Rage hakuzungumzia chochote kuhusiana na mazungmzo yake na nyota hao na badala yake alisema kuwa timu yake ilishindwa kupata ushindi kutokana na kuwadharau wapinzani wao.
Alisema kuwa vile walivyotarajia sivyo, kwani wamekutana na mazingira tofauti na si Comoro ile waliyokuwa wakiifikiria.
"Mechi ilikuwa ngumu tofauti na tulivyokuwa tunafikiria, wachezaji wamestuka wakati muda ukiwa umeshakwisha, wachezaji wa Comoro sasa ni wazuri na wanacheza soka la kuelewana," aliongeza Rage.
Simba inarejea Dar es Salaam leo saa 8:30 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Comoro.
Wakati huo huo, kocha wa Simba, Patrick Phiri amesema kuwa hatarudia kosa katika mechi ya marudiano kwa kufanya maandalizi mazuri zaidi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Phiri alisema kuwa wachezaji wake hawakujiandaa kukutana na ushindani mkubwa, lakini hali hiyo imewapa fundisho na watakuwa makini zaidi pindi watakaporudiana.
Phiri aliongeza kuwa sare si mbaya sana, ingawa imewaweka katika hali ngumu na kutakiwa kufanya juhudi zaidi.
Alisema vilevile kuwa, kutokuwa na mazoezi ya pamoja kwa muda mrefu ni sababu nyingine iliyokifanya kikosi chake kishindwe kucheza soka la kuelewana na kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara.
"Mechi ilikuwa ngumu, tumekutana na ushindani ambao hatukuutarajia, lakini ndio soka... tumejifunza na tutapambana nao tukirejea Dar es Salaam," alisema Phiri.
Aliongeza kuwa kucheza mechi nyingi mfululizo za kirafiki na mashindano pia imesababisha baadhi ya nyota wake kuchoka lakini sasa baada ya ligi kuanza, anaamini watakuwa na muda wa kupumzika.
"Lakini naona ratiba bado ni ngumu kwa Simba,tukiitoa Elan tutacheza na Yanga Machi 5 halafu tunasafiri kwenda kuivaa TP Mazembe, hapo pia tutakuwa tunahitaji kujituma ili tusipoteze mechi zote," aliongeza.
Naye kocha wa Elan, Ayouba, alisema juzi kuwa wachezaji wake walijiandaa vyema na lengo ni kufika hatua ya makundi.
Alisema kuwa lengo lao ni kufanya vizuri na ndio sababu ilifanya usajili mzuri baada ya kutwaa ubingwa wa Comoro Oktoba mwaka jana.
Mechi kati ya Simba na wenyeji wao Elan ilichezwa kwenye Uwanja wa Cheikh Said Mohammed uliopo katika mji wa Mitsamiouli, Moroni katika kisiwa cha Ngazija.