Abiria 157 waliokuwa wakisafiri kwa boti kutoka Ikola wilaya ya Mpanda Mkoa wa Rukwa kuelekea Kigoma, wamenusurika kufa baada ya kukumbwa na dhoruba kali ziwani na injini ya boti hiyo kuharibika.
Boti hiyo ya abiria inayoitwa Pamba Nyepesi, ina uwezo wa kubeba abiria 50 lakini ilikuwa na abiria 157 na gunia mia mbili za bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchele, maharage, samaki na dagaa.
Mmoja wa abiria walionusurika, Juma Mswahili, alisema
hali ilikuwa mbaya kuanzia maeneo ya Lubengela hadi Herembe baada ya injini kuharibika ambapo ili kujiokoa walilazimika kutupa mizigo ziwani ili kupunguza uzito hadi walipookolewa.
“Ndugu waandishi tulianza kupigwa na mawimbi katika maeneo ya Lubengela hali ilikuwa mbaya, tulikata tamaa, tulijua tunakufa, ikabidi tuanze kutupa mizigo ziwani, mimi nimetupa gunia zangu nne za dagaa,”alisema Mswahili.
Abiria mwingine katika boti hiyo, Maria Stanslaus, alisema bila ya kutupa mizigo boti hiyo ilikuwa inazama na wengepoteza maisha.
“Tulianza kupiga simu, mimi nilimpigia mume wangu yuko mjini ili awaambie polisi waje kutuokoa, baada ya kuona kimya akapigiwa Mbunge Peter Serukamba, naye akamwambia Mkuu wa Polisi wa Mkoa ndo ikaja boti ndogo kutuokoa,” alisema.
Kutokana na tatizo hilo, polisi walipata wakati mgumu baada ya wananchi waliofurika katika bandari ndogo ya Kibirizi na Ujiji, kuanza kuhoji kuchelewa kwa Jeshi hilo kuokoa watu hadi chama cha maboti kilipopeleka injini nyingine na kuwezesha abiria hao kuendelea na safari hadi mjini Kigoma.
Kwa upande wake, nahodha wa boti hiyo, Deo Bonifasi, alisema wanalazimika kubeba abiria wengi na mizigo kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika ambao wanategemea boti hizo kwa usafiri baada ya meli za Mv Mwongozo na Liemba kupunguza safari zake.
“Vijiji vya ziwani huko hakuna usafriri, kwa hiyo wakiona boti tu, watu wanajazana na ni ngumu sana kuwaacha, watu wanakaa wiki wanasubiri usafiri ambao haupo, ni kweli boti yangu ina leseni ya kubeba abiria 50 lakini niwaacheje watu? Alisema nahodha wa boti hiyo.
Alisema wingi wa abiria na mizigo katika ukanda huo, unatokana na kupunguzwa kwa safari za meli za MV Liemba na MV Mwongozo, ambazo sasa zinafanya safari mara moja kwa mwezi katika ziwa Tanganyika Kigoma hadi Mpulungu Zambia badala ya safari nne kwa mwezi za awali.
Naye Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Iroga Nashon, alisema pamoja na uchunguzi wa awali kuonyesha kuwa boti hiyo ilizidisha uzito imegundulika kuwa haikuwa na vifaa vya uokoaji ambapo ilikuwa na maboya thelathini tu ya kujiokoa na kwamba watatoa taarifa kamili Jumatatu mara baada ya uchunguzi kukamilika.