Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema hakuna kiongozi ndani ya Jeshi hilo atakayejiuzulu kufuatia vifo vya watu 21 na majeruhi 300 katika milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, kwa kuwa nafasi hizo si za kisiasa.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Usalama na Utambuzi Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, Brigedia Jenerali, Paul Mella, wakati akizungumza na Wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.

Brigedia Jenerali Mella alimwakilisha Mkuu wa Jeshi hilo, Jenerali Davis Mwamunyange, ambaye awali ilitarajiwa kuwa ndiye angezungumza, lakini ilielezwa baadae kuwa ameitwa ghafla kwenye majukumu mengine.
Dhumuni la mkutano huo ilikuwa kueleza mtiririko wa tukio zima la milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi hiyo ya Gongo la Mboto 511 KJ, iliyoko umbali wa kilomita 16 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Mella alisema wanaomtaka Mkuu wa Jeshi hilo, Jenerali Mwamunyange ajiuzulu hawajui Sheria ya Usalama wa Taifa namba 24 ya mwka 1976 na kueleza kuwa wanapaswa kuisoma kabla ya kutoa maoni yao.
“Sisi sio wafanyakazi na ndiyo maana huwezi kusikia Jeshi limegoma, sisi hatuna vyama vya wafanyakazi kama nyinyi kwa hiyo hizi nafasi za kijeshi si za kisiasa au mashirika ya umma na taratibu za kuingia na kutoka jeshini zinajulikana watu wazisome ziko wazi,” alisema Brigedia Jenerali Mella.
Alisema kuna mambo mengi mazuri ambayo Jeshi hilo linafanya lakini hayawekwi wazi kama yanavyoandikwa mambo mabaya inapotokea milipuko ya mabomu.
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, hivi jamani Jeshi limefanya mangapi nchi hii, kule Kilosa wakati wa mafuriko ile reli ilijengwa na wanajeshi ndani ya muda mfupi, wanajeshi wakati wote wako kwenye hatari, msidhani tuna raha, kwa hiyo mnapoandika mabaya yetu basi na mazuri msiyasahau mbona yako mengi,” alisema
“Fikiria wakati milipuko ikiendelea sisi tuliingia mle ndani lengo ikiwa ni kuangalia namna ya kuzima moto uliokuwa ukiendelea kuwaka lakini nyinyi mngekuwepo tukawaambia tuingie wote wengi wenu msingekubali,” alisema na kusababisha kicheko.
Alisema matukio ya ajali kama hizo yamekuwa yakitokea katika mataifa mbalimbali duniani ila tofauti na Tanzania ni kwamba kwenye nchi hizo yamekuwa hayawekwi wazi na inakuwa siri.
Kuhusu milipuko ilivyoanza, alisema siku ya tukio askari waliokuwa eneo kambini, walisikia milio midogo midogo ya milipuko na ilipozidi waliondoka eneo hilo kwenda kutoa taarifa kwa viongozi wa kikosi na hatimaye Makao Makuu (Ngome) ilifahamishwa kuhusu tukio hilo.
Alisema baada ya hapo, maofisa na wapiganaji walikwenda eneo la tukio kwa ajili ya kusaidia kuzima moto ambao wakati huo ulikuwa ukiendelea.
Alisema mlipuko ilitulia majira ya saa 10:30 usiku na wakati huo tayari wananchi wapatao 4,000 walishakimbia maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ya wazi.
Alisema ingawa hawana idadi kamili ya nyumba zilizoharibika lakini kuna nyumba nne ambazo zimeteketea kabisa kwa milipuko hiyo.
Alisema katika purukushani za kujiokoa, maofisa na wapiganaji wanne walijeruhiwa lakini hadi ssa hali zao zinaendelea vizuri.
Alisema katika tukio hilo, maghala 23 ya kuhifadhia mabomu yaliteketea kabisa na mabweni wanayoishi wanajeshi ambao hawajaoa yaliteketea yakiwemo magari manne makubwa ya kijeshi.
“Hili ni janga kubwa la kitaifa ambalo halikutarajiwa, pia chanzo cha milipuko hakijajulikana maana vyanzo vinaweza kuwa vingi, uzembe au hali ya hewa, lakini uchunguzi ukishakamilika tutajua, wananchi tuwe na subira tutakuwa tukiendelea kutoa taarifa kadri tutakavyokuwa tunazipata,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu tume ya Mbagala, alisema majibu ya tume ile ni kwa matumizi ya Jeshi na si rahisi kuwekwa wazi kwa raia.
Naye Mkaguzi Mkuu wa Jeshi, Brigedia Jenerali Leonard Mdeme, alisema iwapo serikali itaamua kambi hiyo ihamishiwe sehemu yoyote hilo litatekelezwa ili mradi litakuwa na maslahi kwa taifa.
“Serikali ikiamua kuwa kambi ihamie kisiwani au wapi, hilo linawezekana lakini kama litazingatia maslahi na usalama wa nchi, maana serikali ikiamua inawezekana,” alisema.
Alisema inawezekana pia wananchi nao wakaondolewa karibu na makambi kwa ajili ya usalama wao iwapo itaonekana inafaa kufanya hivyo.
“Wakati naingia jeshini mwaka 1973 Lugalo ilikuwa mbali sana na Kariakoo, Gongo la Mboto kulikuwa hawaishi watu kabisa, unajua kuhamisha vikosi ni rahisi lakini lazima ieleweke kuwa vikosi hivi mkao wake unasababu zake kiulinzi, serikali ikiamua inawezekana ila hatua za namna hiyo zizingatie maslahi ya kiulinzi,” alisisitiza.
Akizungumzia historia ya kambi hiyo, Brigedia Jenerali Mella alisema ilihamishiwa eneo hilo mwaka 1976 ikitokea Kunduchi na Lugalo na sababu kubwa ya kulipeleka eneo hilo ni kwamba wakati huo hakukuwa na watu karibu na ilikuwa mbali na katikati ya Jiji.
Alisema ilionekana ni busara kuweka kambi hiyo eneo hilo kwa kuwa ni karibu na reli, barabara na usafiri wa anga mambo ambayo ni muhimu katika suala la usalama.
Alisema kambi hiyo ni ghala kubwa la kuhifadhia zana na vifaa mchanganyiko vya kijeshi na kuvigawa kwa vikosi vingine katika maeneo mbalimbali hapa nchini.