Asilimia 80 ya taka ngumu na zile za majumbani zinazozalishwa kila siku mijini na kwenye maji hazitupwi katika madampo, hali inayochangia uchafu.
Akizindua kampeni ya kuhamasisha usafi wa miji na majiji nchi nzima jana jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alisema takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 20 pekee ya taka zinazozalishwa ndizo zinatupwa kwenye maeneo yanayohusika.
Kampeni hiyo imetangaza kwamba kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi itakuwa siku ya usafi.
Dk. Bilal alisema taka nyingi hutupwa katika misingi isiyofaa kimazingira na kusababisha matatizo ya afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara.
“Mara nyingi aina mbalimbali za taka ngumu huchanganywa pamoja na kutupwa hovyo, hii inatokana na kuwepo kwa uelewa mdogo wa jamii na mfumo hafifu wa usimamizi wa taka ngumu,” alisema Dk. Bilal
Alisema aina nyingine za taka zinazozalishwa mjini ni maji taka yanayotoka vyooni, viwandani na mifereji ya maji ya mvua.
Alifafanua kuwa asilimia 80 ya wakazi wa mjini wanatumia vyoo vya shimo huku miongoni mwake vikiwa havikidhi ubora unaotakiwa na kuchangia uchafuzi wa vyanzo vya maji, mazingira na usalama wa afya ya jamii kwa ujumla.
Kufuatia hali hiyo, aliwasihi wananchi washiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa ni jambo la msingi wa afya na maendeleo ya jamii yeyote.
“Katika kuipa kipaumbele kampeni hii na kuifanya endelevu tumeadhimia kufanyika kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huviza, alisema lengo la kampeni hiyo endelevu ni kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira.
Dk. Huviza alisema uchomaji holela wa taka ngumu unaharibu gesi joto na kupelekea mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukosefu wa mvua.
Alisema ingawa serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki bado inatumika jambo ambalo linahatarisha usalama wa mazingira na afya kwa jamii.
“Tutatembelea viwanda ili tuone ni namna gani wanaweza kukabiliana na maji taka yenye sumu katika viwanda hivyo hayaathiri jamii,” alisema Dk. Huviza.