SPIKA wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, amewaonya wabunge kwa kusema, Bunge si uwanja wa siasa hivyo hata wabunge wenye hasira wazitoe bungeni na si nje ya Bunge.
Makinda amesema, wabunge wenye vituko wavitoe bungeni na hatakuwa na uadui nao. Makinda ametoa onyo na msimamo huo leo bungeni mjini Dodoma na kubainisha kwamba, kwa mujibu wa kanuni ya nane ya Bunge la Tanzania, yeye ni Spika wa Bunge na si Spika wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au chama chochote cha siasa.
Amewataka wabunge wafanye kazi zao kwa mujibu wa kanuni za Bunge na kama wana shida waziseme bungeni na si vinginevyo.
“Wewe kama una shida yako sema hapa…huu si uwanja wa siasa” amesema Makinda muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuahirisha mkutano wa pili wa Bunge hadi Aprili tano mwaka huu.
Makinda amesema, anataka wabunge wawe huru, na wawe na uwezo wa kuuliza maswali na kujadili hoja mbalimbali.
Amewasifu wabunge kwa kufanya kazi vizuri, na kwamba, wamejitahidi kuzielewa kanuni za Bunge.
Ameshukuru kwa kupata changamoto wakati wa kuliongoza Bunge, na amesema, zimemuimarisha kwa kuwa amejifunza zaidi.
Makinda amesema, wabunge ni wamoja hivyo hata Mbunge akienda na vituko vyake bungeni, wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge wanaendelea kuwa wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wakanywe chai pamoja, waendelee na kazi.
Amewaeleza wabunge kuwa, ataendelea kuongoza Bunge kwa mujibu wa kanuni za Bunge,hivyo yanayotokea bungeni ni ya bungeni, wasiwe na kinyongo nae.
Wakati anatoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge, Waziri Mkuu amesema, tangu Bunge la 10 lianze kazi amegundua kuna wabunge mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali wakiwemo wasomi wa ngazi zote, vijana na wazee.
Pinda amesema,ana imani kwamba, wabunge hao watatumia utaalamu, umahiri na uwezo walionao kuijenga nchi yetu, na kuwasaidia Watanzania kutoka walipo ili kuleta maendeleo ya nchi yetu.
“Wananchi waliotuchagua wanatutegemea, nawaomba tutangulize uzalendo katika kila jambo tufanyalo kwa manufaa ya taifa letu na watu wake badala ya ushabiki wa kisiasa.
“Nawaomba tuweke maslahi ya Watanzania na taifa mbele,tudumishe amani na utulivu, tupuuze sera zozote za kudhoofisha utaifa wetu kama Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile, iwe ya kikabila, imani za dini, rangi au kwa itikadi za kisiasa” amesema Waziri Mkuu.
Pinda amesema, dhamira ya kila Mbunge iwe ni kukuza uchumi wa nchi yetu na kuondoa umasikini ili kuwaletea wananchi maendeleo na maisha mazuri.
“Tufanye kazi kwa bidii, juhudi, maarifa na ubunifu zaidi. Mimi naamini kuwa, kwa ushirikiano wa Bunge hili na wananchi kwa ujumla tutaweza kutimiza matarajio ya wananchi waliotuchagua na matarajio ya Watanzania wote”amesema Pinda.
0 Comments