MKURUGENZI Mkuu wa mabingwa wa mipasho, Jahazi Modern Taarab, Mzee Yussuf ‘Mfalme’ amebainisha kuwa hivi sasa yuko fiti na kwamba hivi karibuni ataanza kuonekana kwenye maonyesho mbalimbali ya kundi lake hilo.
Akizungumza kisiwani Unguja juzi, Yussuf alisema, onyesho lake la kwanza kupanda jukwaani litakuwa ni lile litakalofanyika siku ya mkesha wa Siku ya Wapendanao ‘Valentine Day’, Februari 13, kwenye ukumbi wa Travertine Hotel, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Alisema, katika onyesho hilo, pamoja na burudani nyingine zote, atawafariji mashabiki waliomkosa kwa kipindi kirefu, kwa kuimba vibao vyake vyote alivyovifyatua tangu alipoanzisha kundi la Jahazi Modern.

“Hivi sasa ninaendelea vema na wiki ijayo nitarudi hospitali kufungua hii ‘POP’ ambapo baada ya hapo nitakuwa huru kuanza kazi jukwaani,” alisema Yussuf ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Yanga.
Akizungumzia zaidi onyesho lake hilo la kwanza kupanda jukwaani, Yussuf alisema kuwa, ana hakika litajaa msisimko wa aina yake, kwani atashiriki pamoja na wanenguaji wa kundi lake kumwaga shoo kabambe.
Aidha, Yussuf alivitaja baadhi ya vibao anavyotarajia kuviimba katika onyesho hilo kuwa ni ‘VIP Nafasi Yangu’, ‘Nakula kwa Nakshi Nakshi’, ‘Tupendane Wabaya Waulizane’, ‘Daktari wa Mapenzi’ pamoja na ‘My Valentine’.
Alisema kuwa, kibao ‘My Valentine’ kitakuwa maalum siku hiyo, ambako atakiimba akiwa amekaa chini mbele ya jukwaa kuonyesha kuwa hata yeye pia alikuwa akiwakumbuka mno mashabiki pamoja na wapenzi wake.
“Nawaomba mashabiki pamoja na wapenzi wangu wote wafike kwa wingi katika onyesho hilo nililoliandaa kwa ajili yao,” alisema Yussuf, mahiri kwa uimbaji, utunzi na upapasaji kinanda.
Kadhalika, Yussuf alieleza kuwa, Valentine Day yaani Februari 14, burudani hiyo itahamia Temeke jijini Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa Buliyaga Bar.