Serikali ya Italia inajitahidi kukabiliana na mgogoro uliopo katika kisiwa kidogo cha Lampedusa baada ya wahamiaji 1,000 kuwasili kutoka Tunisia.
Kituo kimoja kilichoandaliwa mahsusi kwa ajili ya watu 850 kimeripotiwa kufurika.Tunisia imeikatalia Italia kusambaza polisi wake kwenye eneo lao.
Zaidi ya wahamiaji 4,000 wanaripotiwa kuwasili Lampedusa katika siku chache zilizopita.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Baroness Ashton kwa sasa yupo Tunis kujadili suala hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Franco Frattini naye anatarajiwa kufika Tunis siku ya Jumatatu.
Gazeti la Italy La Repubblica limeripoti kuwa alijadili kuhusu mmiminiko huo wa wahamiaji na Lady Ashton na kutoa wito wa shirika la mipaka la Umoja wa Ulaya Frontex kujihusisha, kusaidia kupiga doria kwenye maji ya Lampedusa.
Siku ya Jumamosi Italia ilitangaza dharura ya masuala ya kibinadamu na kutoa wito wa kupata msaada kutoka Umoja wa Ulaya.
Msemaji wa shirika la kimataifa la uhamiaji, Simona Moscarelli, alisema Italia lazima iwahamishe wahamiaji kutoka Lampedusa kwenda upande wa bara wa Italia haraka iwezekanavyo.
0 Comments