Mwanasoka mashuhuri wa Brazil, Ronaldo, ambae aliisaidia nchi yake kunyakua kombe la dunia 1994 na 2002, amethibitisha kuwa anajiuzulu kucheza soka.
Anaacha kandanda akiwa na rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika fainali za kombe la dunia kushinda mchezaji mwingine yeyote.

Lakini sasa akiwa na umri wa miaka 34, Ronaldo anasema mwili wake haumruhusu tena kuendelea.
Katika kipindi cha miaka 18 iliyopita Ronaldo amefungia Brazil mabao 62 katika mechi za kimataifa,na kati hayo mabao 15 katika fainali za kombe la dunia, hii ikiwa ni rikodi.
Alionyesha ustadi wake kwa vilabu mashuhuri barani Ulaya, ikiwemo Barcelona, Real Madrid na Inter Milan.
Ametunukiwa tuzo ya FIFA ya kuwa mchezaji bora duniani mara tatu.
Alirejea Brazil akitumaini kukamilisha msimu wa mwisho katika michuano ya klabu.
Lakini maumivu yake na hali ya mwili wake ambayo ilimfanya asiweze kupunguza uzito wa mwili wake hatimaye vilimkatisha tamaa na akaamua asalimu amri.