Akaunti ya kamishna iliyochezewa ni ya benki ya CRDB tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo katika sakata hilo, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru) nayo ilishaanza mchakato wa kuwahoji maofisa wa CRDB na TRA kuhusiana na mchezo huo mchafu.
Wakizungunza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, Kamishana wa TRA, Henry Kitilya na Meneja wa TRA mkoani hapa, Patiencia Minga, walithibitisha kufukuzwa kazi kwa watumishi hao lakini hawakuwa tayari kuwataja kwa majina.
“Elewa kuwa tumewafukuza kazi...kuhusu hatua nyingine hiyo siyo kazi yetu au unataka tuwafuate hadi majumbani kwao kuwasakama ndio mjue TRA tumechukua hatua,” alisema Kitilya wakati Minga alisema kuwa hana la kusema baada ya kamishna kutoa uamuzi huo wa kuwatimua kazi wafanyakazi wake.
Benki ya CRDB mkoani Kilimanjaro ilishaliomba Jeshi la Polisi mkoani hapa na Takukuru kuifikisha mahakamani benki hiyo ili ikatoe vielelezo vyote vya jinsi akaunti ya kamishina ilivyochezewa na kuingiza kodi hewa serikalini.
Meneja wa benki hiyo mkoani hapa, Francisi Mollel, aliieleza NIPASHE jana kwa njia ya simu kuwa madai ya baadhi ya maofisa wa TRA na mawakala wa kampuni za kuhakiki mizigo katika kituo cha Holili kuwa benki hiyo inahusika hazikubaliki.
Alisema CRDB ni benki makini kuliko benki nyingine hivyo hawawezi kuchezea akaunti ya kamishina na kuwa waliocheza mchezo huo ni TRA wenyewe na kwamba kama TRA, Polisi na Takukuru wakiwahitaji mahakamani kama mashahidi watakwenda kutoa ushahidi.
"Tunaomba hao Takukuru, TRA au Polisi watufikishe mahakamani ndipo wateja wetu watafahamu kuwa CRDB tuko makini katika masuala ya kifedha," alisema kufuatia taarifa kuwa TRA ilishaandika barua kuwa endapo mteja akakosea kuweka fedha katika akaunti ya kamishina, CRDB isitoe fedha hadi kibali cha kamishna.
Ilidaiwa kuwa waliokuwa wakicheza na akaunti ya kamishna walikuwa wakiweka fedha CRDB kisha kudai kuwa walikosea akaunti hivyo hurudishiwa fedha zao na kuchukua nakala ya kuweka fedha hizo na kuipeleka TRA na hivyo kuthibitisha kuwa alishalipia fedha katika akaunti ya kamishna kwa kuwa TRA wanahitaji nakala ya malipo ya CRDB.
0 Comments