Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeungana na Rais Jakaya Kikwete, katika kulaani vikali maandamano yaliyofanywa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa madai kwamba yanachochea uasi na machafuko nchini.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Kapteni mstaafu John Chiligati, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ndogo Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Chiligati alisema kufanya maandamano si tatizo kwa kuwa ni haki ya kikatiba, isipokuwa kauli zinazotolewa katika maandamano hayo ni mbaya na zina lengo la kuhamasisha wananchi kufanya vurugu.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, alisema maandamano yanayofanywa na Chadema yana lengo la kuwachochea wananchi kuichukia serikali yao na kwamba yanaweza kuvunja amani ya nchi.
Rais Kikwete alisema uamuzi wa wananchi ulishafanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka jana kwa kuichagua CCM.
“Tangu viongozi wa Chadema waanze ziara yao katika mikoa ya Kanda ya Ziwa tumeshuhudia wakitoa kauli za kupotosha umma na zenye kuchochea uasi, ambazo zinawataka wananchi wafanye fujo kama Tunisia na Libya na kuhamasisha nchi isitawalike na Rais aondoke madarakani,” alisema Chiligati.
Chiligati alisema wanaunga mkono hotuba ya Rais aliyoitoa mwishoni mwa Februari, mwaka huu ambapo alikemea kauli hizo za uchochezi ili kuinusuru nchi kuingia katika machafuko na kwamba zinavunja sheria na Katiba ya nchi.
“Tunaunga mkono kauli ya Rais aliyoitoa mwishoni mwa mwezi Februari kukemea kauli hizi ili kuinusuru nchi yetu na machafuko yanayoweza kutokea na pia kauli hizi zinazotolewa na Chadema ni ukiukwaji wa sheria na Katiba ya nchi,” alisema.
Aliongeza: “Hotuba iliyotolewa na Rais imepongezwa na wananchi wengi wapenda amani, lakini cha kushangaza tumesikia majibu ya Dk. Willibrod Slaa (Katibu Mkuu) na Freeman Mbowe (Mwenyekiti) wa chama hicho wakisema wataendelea na kauli za kuchochea vurugu kupitia kauli zao tunazowasikia wakisema wembe ni ule ule hadi kieleweke, hii inamaanisha wataendelea na kauli zao za kuchochea vurugu na nchi isitawalike,” alisema.
Chiligati alisema kipindi cha malumbano, mivutano, kuitana majina ya kejeli kimepita na hivi sasa cha muhimu ni kuangalia namna ya kutekeleza ahadi zilizotolewa kupitia Ilani za Uchaguzi za vyama vya siasa.
Alisema hatua ya Dk. Slaa kuendeleza malumbano na uchochezi kunaonyesha kuwa hajakubaliana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwishoni mwa mwaka jana, hivyo anaendeleza kwa vitendo uamuzi wa Chadema wa kutomtambua Rais Jakaya Kikwete.
Chiligati alimfananisha Dk. Slaa na Jonas Savimbi wa Angola, aliyekuwa kiongozi wa Chama Cha Unita.
“Hatutaki usavimbi hapa Tanzania, Dk. Slaa akubali ameshindwa uchaguzi na ajipange kwa uchaguzi ujao, aboreshe sera zake na chama chake sio kuchochea uzushi dhidi ya Rais aliyeko madarakani kama ana mawazo au mapendekezo ya kusaidia ufumbuzi wa matatizo ya wananchi atumie wabunge wa chama chake la sivyo hizo anazotumia ni ghiliba ambazo Watanzania watazigundua tu,” alisema.
“Tunapenda tueleweke kuwa hatusemi vyama vya upinzani visiikosoe serikali, hapana, uhuru upo wa kutosha ila iwe kwa lugha ya kiungwana, sio matusi, kudhalilishana wala uchochezi,” aliongeza.
Aidha, aliwaonya wanasiasa kutoipeleka nchi katika matatizo na kuvitaka vyombo vya dola kumchukulia hatua mtu yeyote anayechezea amani na usalama wa nchi kupitia kauli au vitendo bila kujali chama chake.
Akizungumzia suala la kampuni ya kufufua umeme ya Dowans Tanzania Limited, Chiligati alisema kati ya mambo ambayo Chadema inapotosha umma ni tafsiri ya suala la malipo ya deni la Sh. bilioni 94 ambalo wamekuwa wakilichukulia kana kwamba serikali ndio iliamua kwa furaha kulipa.
Alisema lazima ieleweke kuwa suala la malipo ya deni hilo, lilitokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) na sio serikali wala CCM.
Chadema ilipoanza maandamano yake ya amani katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Kagera Februari 24 kwa lengo la kuishinikiza serikali isiilipe Dowans, kushusha gharama za umeme na kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, baada ya Rais Kikwete kukishutumu chama hicho kwa kuchochea vurugu, baadhi ya wanasiasa wamejitokeza kuunga mkono hotuba yake.
Miongoni mwa waliomuunga mkono na kukishutumu Chadema ni Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema; Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na mwanaharakati wa Amani, Risasi Mwaulanga.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, ameitishia Chadema kuwa itafika mahali serikali itakosa uvumilivu ikiwa kitaendelea kufanya maandamano ya uchochezi.
Licha ya Chadema kulalamikiwa kutumia mikutano na maandamano kuchochea vurugu, ziara ya Operesheni Sangara ilihitimishwa juzi mkoani Kagera bila kuwepo tukio lolote la kuvunja amani.
Katika miji yote ya makao makuu ya mikoa na wilaya wananchi walijitokeza kwa wingi kushiriki maandamano na mikutano ya hadhara bila kufanya vitendo vyovyote vya kuvunja amani.
CCK yaunga mkono maandamano
Wakati CCM ikiyalaani maandamano ya Chadema kimesema kuwa Chama Cha Kijamii (CCK) kimeikosoa hotuba ya Rais Kikwete ya mwisho wa mwezi uliopita na kukishambulia Chadema.
Mwenyekiti wa chama hicho, Cistantine Akitanda, alisema haipendezi Rais wa nchi aliyepewa madaraka na wananchi kuzungumza akiihofia Chadema kwamba kinafanya matendo ya kuvunja amani ya nchi bila ya kuchukua hatua zinazostahili.
“Suala la amani ya nchi si la kucompromise (kutafuta ridhaa au maafikiano). Ni suala linalohitaji vyombo vinavyohusika kisheria kuchukua hatua mara moja pale itakapothibitika kwamba Chadema wamefanya vitendo vya kuvuruga amani ya nchi,” alisema Akitanda.
Aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa amani ya nchi ni muhimu kuliko kitu kingine chochote kile kwa kuwa watu na vitu vitapita, lakini Tanzania itaendelea kubaki.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Renatus Muabhi, alisema pamoja na kutoa msimamo huo, bado wanamshauri Rais Kikwete kuwachukulia hatua za kinidhamu watu wake wa karibu ambao wametuhumiwa muda mrefu.
“Tunamwambia Rais awafukuze watu wake wa karibu ambao vyama vya siasa na wananchi wamekuwa wakiwasema kwa muda mrefu kuwa wameiletea nchi matatizo mengi. Mtu kama Rostam Aziz, Andrew Chenge na akina Msabaha ni muhimu akawachukulia hatua kwani hawa ndio wanaosababisha wananchi waichukie serikali,” alisema.
0 Comments