Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, alimtaja askari huyo kuwa ni Konstebo Selemani Lukuta.
Athumani, alisema askari huyo alijipiga risasi juzi saa 12:00 jioni muda mfupi baada ya kukabidhiwa bunduki aina ya SMG na risasi 30 tayari kwenda kufanya doria.
Kamanda Athumani alisema
mpaka sasa haijafahamika sababu ya kujiua kwake kwa kuwa kabla ya kujiua hakuonyesha dalili zozote za kuwa na tatizo.Akifafanua kuhusu tukio hilo, Kamanda huyo alisema siku ya tukio polisi huyo akiwa na askari wenzake walikwenda katika ghala la kutunzia silaha na baada ya kukaguliwa kama ilivyo kawaida hakuonekana kuwa na tatizo lolote na hivyo alikabidhiwa silaha pamoja na risasi zake na kisha walipewa maelekezo ya mkuu wao wa zamu kuhusu kazi za siku hiyo.
“Baada ya kupewa maelekezo ya kazi kama ilivyo kawaida ya siku zote, ghafla polisi huyo alielekeza silaha yake sehemu ya shingoni na kujipiga risasi ambayo ilifumua kichwa chake na akafa papo hapo. Haijafahamika sababu yoyote iliyosababisha kuchukua uamuzi huo,Alisema.
Alisema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo, kuna tetesi zinazodai kuwa askari huyo aliamua kujiua baada ya kupangwa doria mara mbili kwa siku moja.
Hata hivyo, Kamanda huyo alikanusha taarifa hizo na kusisitiza kuwa hazina ukweli wowote.
Alisema hata wenzake aliokuwa amepangwa nao kwenye doria hiyo juzi walikuwa na zamu nyingine nyakati za asubuhi.
" Huyu ni mmoja wa vijana wetu walioingia jeshini mwaka jana hivyo ana mwaka mmoja tu kazini na utaratibu huo sio mgeni kwake," alisema.
Alisema mwili wa marehemu ulitarajiwa kusafirishwa jana kupelekwa nyumbani kwao mkoani Tabora ambako leo anatarajiwa kuzikwa.
0 Comments