MWANAMUZIKI mkongwe nchini Muhidin Gurumo amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kumtembelea hospitalini alikokuwa amelazwa na pia ametangaza kwamba atastaafu muziki mwaka 2013. Katika mahojiano na Redio One, Dar es Salaam, Gurumo amesema Kikwete alimtembelea akiwa hospitalini hivi karibuni na ujio wake ulimuwezesha kuhudumiwa vema na kupona haraka.
“Napenda kumshukuru Rais Kikwete, ni mtu mwenye roho nzuri mno,” alisema. Gurumo ambaye amejipatia umaarufu mkubwa katika tasnia ya muziki nchini tangu mwaka 1961 alipoanza kuimba alisema iwapo Mungu atamuweka hai amepanga kustaafu muziki mwaka 2013.
“Nilikuwa mgonjwa, lakini naendelea vizuri kwa sasa, nafikiria kustaafu mwaka 2013 ili kuwaachia vijana, lakini nitakuwa tayari kusaidia kama kuna mtu atahitaji msaada wangu,” alisema.
Gurumo aliwaasa wanamuziki wa sasa kufanya kazi kwa bidii na kulinda fani hiyo.
“Wanamuziki wa siku hizi wanapenda kurap mimi sioni maana, wanaharibu uimbaji ingawa wanasema wanafanya hivyo badala ya saxophone ambazo sisi tulikuwa tunatumia,” alisema.
Mkongwe huyo alisema anavutiwa na uimbaji wa Cosmas Chidumule, marehemu Moshi William na Hussein Jumbe ambaye alimuelezea kuwa ni mwanamuziki mzuri, lakini hana bahati.
0 Comments