Rais Jakaya Kikwete, amesema yuko tayari kuliamuru Jeshi kuingia kwenye hifadhi za wanyamapori kupambana na majangili iwapo Wizara ya Maliasili na Utalii itamhakikishia kuwa imezidiwa nguvu na watu hao.
Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na viongozi, watendaji na wafanyakazi wa wizara hiyo alipotembelea wizarani hapo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Januari, 2006, ikiwa ni mwaka baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi.
Rais Kikwete alisema kuwa ana hofu kwamba wizara hiyo imezidiwa nguvu na majangili katika hifadhi hizo kutokana na matukio kadhaa ya kuuawa wanyamapori na uporaji wa pembe za ndovu kuongezeka.
“Ujangili hamjazidiwa?” Alihoji Rais Kikwete na kujibiwa na Waziri wa Wizara hiyo, Ezekiel Maige kuwa: “Hatujazidiwa, tofauti na miaka iliyopita.”
Hata hivyo, jibu hilo la Waziri Maige, ambalo kabla ya kulitoa alisita kidogo, lilimfanya Rais Kikwete kutamka: “Maana naona matukio ya kuuawa tembo na meno ya tembo kutekwa yameongezeka.”
“Je, hamuoni haja kuwashirikisha wenzenu? Kama hili jambo limewazidi kimo semeni, usione haya. Kama mwenendo ni huu tuingize Jeshi, kama tulivyofanya mwaka 1986. Maana haiwezekani kuendelea na hali hii,” alisema Rais Kikwete.
Rais aliongeza: “Mkizidiwa kimo nchi hii inavyo vyombo vingi. Mimi napata hofu kuwa mmezidiwa. Nadhani intelijensia yenu ifanye kazi kujua ndani yenu nani si muadilifu. Mimi ni Commander in Chief (Amiri Jeshi Mkuu) nina majeshi mengi. Lazima tufanye msako tuwakamate watu hawa. Sina hakika kama shughuli hii itaishia kwa askari wa wanyamapori.”
Rais Kikwete pia, aliagiza adhabu dhidi ya majangili, ambayo kwa mujibu wa Waziri Maige kupitia mwanasheria wa wizara hiyo, ni kifungo cha jela kuanzia miezi 12 hadi 36 kutegemea makosa, ziongezwe kwani adhabu ya sasa ni ndogo na haiwezi kukomesha vitendo vya ujangili.
AAGIZA MAOMBI KWA UNESCO YAFUTWE
Pia, aliagiza wizara hiyo kufuta mara moja maombi waliyoyapeleka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kutaka milima ya Tao la Mashariki, inayojumuisha milima ya Uluguru, Udzugwa na Pare, itangazwe kuwa urithi wa dunia.
Rais Kikwete alisema suala hilo halina faida kwa nchi, badala yake ni la hatari kwani linaifanya Unesco kuwa mmiliki wa maeneo hayo na kwamba, maamuzi hayo yalifanywa na wizara bila kumshirikisha Rais.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments