Serikali imesema haina uwezo wa kumaliza makali ya maisha yanayowakabili Watanzania na kumtaka kila mtu ale kwa jasho lake mwenyewe kama maandiko ya Mungu yanavyosema.
Kadhalika, serikali imesema haina mpango wa kupunguza kodi katika mafuta ili kusaidia kushusha bei ya bidhaa hiyo inayozidi kupanda siku hadi siku.(Pichani ni waziri wa Fedha na Uchumi bwana Mustafa Mkulo).
Msimamo huo wa serikali ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kwa waandishi wa habari baada ya waandishi wa habari kumtaka atoe kauli ya serikali kuhusiana na malalamiko ya wananchi kuhusu kasi ya kupanda kwa gharama za maisha nchini.
“Maandiko yanasema kila mtu atakula kwa jasho lake na apigae hodi atafunguliwa, hivyo wananchi wasitegemee unafuu wa maisha utaletwa na serikali,” alisema Waziri Mkulo.
Mkulo alisema hakuna mtu yeyote nchini aliyesababisha kupanda kwa gharama za maisha, bali hali hiyo imetokana na matatizo ya ulimwengu mzima.
“Hata nchi tajiri duniani bado kuna watu maskini wa kutupa ambao wanakaa mitaani kwa ajili ya kuomba omba hivyo sio Tanzania pekee ambayo watu wake wanakabiliwa na tatizo la ugumu wa maisha,” alisema Waziri Mkulo.
KUDHIBITI MFUMUKO WA BEI
Waziri Mkulo akizungumzia mlalamiko kuwa kuna kasi kubwa ya mfumuko wa bei nchini, alisema kuwa serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha mfumuko wa bei hauongezeki zaidi ya asilimia 7.5 ifikapo Juni mwaka huu.
Hivi sasa kiwango cha mfumuko wa bei nchini ni zaidi ya asilimia sita.
Pamoja na kutokueleza hatua ambazo serikali itazichukua kudhibiti mfumuko wa bei, lakini Waziri Mkulo alieleza hatua ya muda mrefu ambayo alisema ni kuwekeza katika sekta ya kilimo na kwamba chakula kikipatikana kwa wingi, hakuna uwezekano wa kuwepo kasi ya mfumuko wa bei.
Alijisifu kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kudhibiti mfumuko wa bei ikilinganishwa na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Waziri Mkulo alisema kiwango cha mfumuko wa bei katika nchi nyingi za Afrika Mashariki ni zaidi ya asilimia 10.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkulo alisema serikali haina mpango wa kupunguza kodi katika mafuta kwa ajili ya kupunguza makali ya maisha.
BARABARA ZATELEKEZWA
Wakati huohuo, imeelezwa kuwa serikali imetelekeza miradi mingi ya barabara ambayo ilitengewa fedha kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge mwaka jana bila ya kutoa maelezo yoyote kwa wabunge.
Mbunge wa Bariadi (Magharibi), Andrew Chenge, alimuomba Mkulo kumpa sababu kwa nini miradi hiyo inashindwa kutekelezwa licha ya kuwa fedha zake zilikwisha kutengwa.
“Mimi naomba ufafanuzi wa Waziri Mkulo ni kwa nini miradi ambayo Bunge lilipitisha fedha zake imeshindwa kutekelezwa kwa wakati,” alisema Chenge katika semina ya wabunge iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkulo juzi na jana alihudhuria semina hiyo na kuelezea vipaumbele vya serikali katika bajeti ijayo ya mwaka 2011/12.
Akijibu swali la Chenge, Waziri Mkulo alisema sababu iliyochangia miradi hiyo kushindwa kutekelezwa kwa wakati ni kutokana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuingia mikataba ya ujenzi wakati hawana fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali ilijikuta ikiwa na miradi mingi kuliko ile iliyoombewa fedha na hivyo kushindwa kuitekeleza kwa wakati kama ilivyotarajiwa.
Hata hivyo, Mkulo aliitakaTanroads kuacha kuingia mikataba ya ujenzi wa barabara kwa kutegemea fedha za bajeti ya serikali inayopitishwa kila mwaka kwa kuwa hali hiyo itazidi kuleta mkanganyiko wa kiutendaji ndani ya serikali.
0 Comments