KITENDO cha binadamu kushindwa kutekeleza majukumu yake na kutumia kilevi kama kichocheo cha nguvu za kutekeleza jambo hilo, ni dalili ya ugonjwa wa akili.
Vile vile, imeelezwa kuwa, tabia ya watu wanaotumia ulevi wa aina mbalimbali kukosa imani na kila mtu kwa kila jambo bila sababu za msingi ni ugonjwa wa akili.
 
Mtaalamu wa magonjwa hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa Sehemu ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Afya ya Akili na Dawa za Kulevya wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Joseph Mbatia alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza  muda mfupi baada ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha jamii kuepukana na ulevi wa pombe wa kupindukia.

Kampeni hiyo itakayoendeshwa na vituo 11 vya redio nchini, vipererushi, magazeti na njia nyingine za mawasiliano ya umma ilizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni na zitadumu kwa miezi sita ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu juu ya madhara ya pombe na kubadili tabia ya ulevi.

Kwa mujibu wa Dk. Mbatia, idadi kubwa ya wagonjwa wa akili waliopo nchini inatokana na ulevi wa kupindukia wa pombe na vileo vingine.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Nyoni alisema pombe ni hatari na haipaswi kuendekezwa kwa kuwa inachochea umasikini kwa kiasi kikubwa, ugomvi katika familia, kusambaa kwa maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na madhara mengine mengi.