TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

VIWANGO VIPYA VYA JUU VYA NAULI ZA MABASI YA DALADALA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekamilisha mchakato na kuridhia viwango vipya vya nauli kwa ajili ya usafiri wa mijini husan katika Jiji la Dar es Salaam. Viwango hivi vipya vimefikiwa baada ya kufuata taratibu za kisheria na za kiutendaji ambazo SUMATRA kama msimamizi na mdhibiti wa sekta ya usafiri wa barabara inapaswa kuzifuata kabla ya kuridhia viwango hivyo. Viwango vya nauli vitaanza kutumika kuanzia tarehe 10 Machi, 2011.

Katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka wa fedha wa 2009/2010, SUMATRA ilipokea maombi rasmi kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa barabara wakiwemo Umoja wa Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA) wakipendekeza mapitio ya viwango vya nauli za mabasi yanayotoa huduma za usafiri mijini (Daladala) kufuatia ongezeko la gharama za uendeshaji kwa mujibu wa mawasilisho yao. Maombi ya wamiliki wa Daladala yalilenga katika kuongeza viwango vya nauli kwa kati ya 172% na 200% ya viwango vya sasa.

Kwa mujibu wa Kifungu Na 18 cha Sheria ya SUMATRA, 2001, SUMATRA iliwashirikisha wadau mbalimbali katika kujadili na kupata maoni yao kuhusu maombi ya wamiliki ya kuongeza viwango vya nauli kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho.

Kwa kuzingatia hoja za waombaji, maoni ya wadau, uchambuzi wa menejimenti, haja ya kupunguza gharama zisizo za lazima za uendeshaji na udhibiti wa vitendo vya uvunjaji wa Sheria na taratibu za uendeshaji shughuli za usafirishaji, Mamlaka ya SUMATRA imeamua kuongeza viwango vya juu vya nauli za Daladala kwa wastani wa 17.9% ambapo kiwango cha nauli kwa abiria kwa kila kilomita kimepanda kutoka Sh 22.9 hadi Sh 27.

Mchanganuo wa viwango vipya vya nauli ni kama ifuatavyo:

1.     Nauli za Daladala – Jiji la Dar es Salaam
Umbali wa Njia
Kiwango Kipya cha Nauli
Mfano wa Njia
Kilomita kati ya 0 – 10
Sh 300
Mbagala – Posta
Kilomita kati ya 0 - 15
Sh 350
Kawe - Kariakoo
Kilomita kati ya 0 - 20
Sh 400
Kimara – Posta
Kilomita kati ya 0 - 25
Sh 500
Tegeta - Kariakoo
Kilomita kati ya 0 - 30
Sh 650
Kibamba - Kariakoo

Nauli ya Mwanafunzi itakuwa Sh 150/= ambayo ni nusu ya nauli ya mtu mzima ya kiwango cha chini cha nauli ya Sh 300/=. Nauli hii itatumika kwa njia zote za Jiji la Dar es Salaam .

Ili kuhakikisha kuwa kuna uwiano kati ya viwango vipya vya nauli na ubora wa huduma ya usafiri, Mamlaka imetoa maagizo kwa wamiliki kuboresha maeneo yanayohusiana na huduma ya usafiri kama ifuatavyo:
(i)                Kufuata Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya usafirishaji abiria
(ii)              Kuandika katika mlango wa kuingia abiria viwango vya nauli inavyotoza katika njia anayotoa huduma ya usafiri
(iii)            Kutoa tiketi kwa kila abiria ikionyesha jina la mmiliki, namba ya usajili wa basi, kituo cha mwanzo na mwisho wa safari, nauli na tarehe ya safari
(iv)            Kuzingatia usafi wa mabasi na sare za wafanyakazi wao, kutotumia wapiga debe, kutotumia lugha chafu, kutokatisha njia na kutowabugudhi wanafunzi 
(v)              Kubeba idadi ya abiria kulingana na uwezo wa basi na kuwepo na nafasi ya kutosha na sehemu ya kushika kwa abiria wanaosimama ndani ya mabasi makubwa
(vi)            Kuhakiksha basi linabeba idadi ya abiria ambao wanapaswa kubebwa kwa mujibu wa idadi iliyoidhinishwa na mtengenezaji wa basi
(vii)          Kuwepo na Bima inayowalinda abiria wote wa basi husika
(viii)        Abiria wanawajibika kurejesha utamaduni wa kupanga mabasi kwa mstari na mabasi nayo yanapaswa kupakia abiria kwa mstari.

Ni vyema ikumbukwe kuwa SUMATRA ina wajibu kisheria kuhakikisha pamoja na mambo mengine kuwa maslahi ya watumiaji na watoa huduma za usafiri yanalindwa ili kuwepo na huduma endelevu ya usafiri ulio bora, salama na wenye kukidhi mahitaji.  Aidha SUMATRA ina jukumu la kujenga na kulinda mazingira mazuri na ya kuvutia kwa watoa huduma ili huduma ya usafiri inayotolewa inakuwa katika kiwango na gharama zinazoendana na huduma zenyewe.

Mamlaka ya SUMATRA inaendelea kuimarisha ushirikiano kwa kufanya kazi kwa karibu  na Mamlaka zingine kama Ofisi ya Mkuu wa Mikoa, Serikali za Mitaa, Mamlaka za Manispaa, Polisi, TBS, TANROADS, Kamisheni ya Bima na wananchi kwa ujumla, katika kuleta mageuzi ya utoaji wa huduma za usafiri wa barabara kwa kiwango cha juu.


Imetolewa na:
David Mziray
Meneja Mawasiliano kwa Umma
3 Machi, 2011