Kiongozi mmoja wa muungano wa wanajeshi wa nchi za magaharibi amesema wamevunja ngome za kikosi cha wanajeshi wa anga wa Libya.
Jemedari Greg Bagwell kutoka Uingereza amesema kikosi hicho hakina nguvu za kuwashambulia raia na hata ndege zao zinazopaa nchini humo.Jemedari Bagwell akizungumza kwenye kituo chao cha kijeshi nchini Italy, ameongeza kuwa wanajeshi wa ardhini watalengwa wakati wowote watakapo shambulia raia.
Ikiwa hii ni siku ya sita tangu mashambulizi hayo yaanze dhidi ya wanajeshi wa Kanali Muammar Gaddafi, bado kuna malumbano kati ya NATO na wanajeshi wengine wanaoshiriki kwenye operesheni hiyo kuhusu nani atakae chukuwa uongozi wa harakati hizo.
Marekani ndio inayoongoza harakati hizo lakini inataka kuachia wadhifa huo haraka iwezekanavyo.
Kumekuwepo na msururu wa mazungumzo kati ya nchi wanachama wa shirika hilo la NATO kuhusu uwezekano kuwa lichukuwe uongozi huo, lakini kuna baadhi ya wanachama wanatashwishi na kuhusika kwao kwenye siasa za nchi za kiarabu.
Kwa sasa mpango uliopo ni kuwa huenda NATO ikachukua jukumu la kupanga operesheni hiyo lakini masuala ya kisiasa kuhusu harakati hizo ziongozwe na jopo linaloshirikisha nchi zaidi.
Uamuzi kamili kuhusu hilo unatarajiwa jummanne ijayo wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi wanachama wa NATO watakutana mjini London Uingereza.
0 Comments