MENEJIMENTI ya Kiwanda cha kutengeza nguo cha African Pride cha Dar es Salaam, jana iliambulia kipigo kikali kutoka kwa wanandugu wa mfanyakazi Ibrahim Othman (61) aliyefia kazini hapo kwa kuangukiwa na ukuta.
Ndugu wa marehemu huyo wamedai kuwa uongozi wa kiwanda hicho umeshindwa kugharamia usafiri wa maiti pamoja na chakula kwa wafiwa.
Mtoto wa marehemu, Khalfan Ibrahim amesema, baba yake ambaye alikuwa msimamizi wa wafanyakazi kiwandani hapo, alikufa Machi 21, mwaka huu saa 10 jioni kwa kuangukiwa na ukuta wakati akisimamia marekebisho katika moja ya jengo la kiwanda hicho kilichopo Shekilango, Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa, jengo hilo limejengwa kwa kiwango duni.
Khalfan amesema, baada ya msiba huo, wanandugu walikutana na uongozi wa kiwanda, ukakubali kutoa fedha za kugharamia kusafirisha maiti, wanandugu pamoja na chakula.
Alisema, baadae uongozi ulibadilika na kudai kuwa utasafirisha maiti huyo na watu watatu peke tu.
Hali hiyo ilizusha mtafaruku miongoni mwa wanandugu hao ambao walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya safari hiyo ya kwenda kumzika marehemu kwao wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Kutokana na hali hiyo, wanandugu walibeba maiti kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, Mwananyamala na kuifikisha ofisini hapo huku wakitishia kuitelekeza hadi Menejimenti itakapobadilika na kukubali kugharamia mahitaji hayo kwa kuwa ndugu yao alifanya kazi kwa miaka saba na alikutwa na mauti kazini.
Katika vurugu hizo zililodumu kwa zaidi ya saa moja hadi askari polisi kuingilia kati, wanandugu hao walikuwa wakitaka kujua ni jinsi gani mwili wa ndugu huyo utasafirishwa na kufikishwa Lushoto kwa kuwa Menejimenti ilisema ingetoa gari aina ya Toyota Pick up ambayo itasafirisha maiti na ndugu watatu peke yake tofauti na makubaliano ya awali ya kutoa basi na chakula kwa wafiwa.
Wakiwa na jazba, wanandugu hao baada ya kufika kiwandani hapo, waliingiza maiti ndani na kutaka kuonana na Mkurugenzi Mtendaji, Meneja Mwajiri aliyetambuliwa kwa jina la Burhan Mbarouk, alijitokeza na kuanza kutoa majibu ambayo hayakuwafurahisha.
Akizungumza na wanandugu hao, Mbarouk aliwaambia kwa kejeli wanandugu hao, “Mmekuja hapa kuna tatizo gani? Kwanza Mkurugenzi hayupo, subirini nje gari inamalizia kuwekwa tairi ili muanze safari.”
Kutokana na maelezo hayo ambayo hayakuwaridhisha wanandugu hao, waliamua kumtoa nje kwa kipigo kikali hadi kuchaniwa fulana akitakiwa kutanguliza utu kwa wafanyakazi pindi wanapopata ajali wakiwa kazini na kuhakikisha kuwa wanapatiwa huduma zinazostahili.
Wakati mwajiri huyo akipatiwa kipigo, walitokea viongozi wawili wenye asili ya Kiasia, ambapo kwa nyakati tofauti nao walipigwa wakidaiwa kuwa chanzo kilichosababisha maiti kutofikishwa Lushoto, hali iliyosababisha kujisalimisha kwa kukimbilia ndani, huku wakitamka kuwa watawapa wanachokitaka.
Baada ya mtafaruku huo, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Nilesh Bhatt alikubali kutoa Sh milioni mbili ili kusafirisha mwili huo pamoja na wanandugu hao, jambo ambalo waliliridhia kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, wafanyakazi wa kiwanda hicho wakizungumza kwa nyakati tofauti bila kutaja majina yao, walikiri kusononeshwa na kitendo hicho cha mwajiri kutokuwajali wanapofikwa na ajali kazini.
0 Comments