POLISI mkoani Lindi, wamemkamata mkazi wa kijiji cha Nanyanje, mjini Lindi, Rashidi Mnyau (36), kwa tuhuma za kumjeruhi mtoto wake, Abdallah Rashidi, kwa kumchoma moto mikononi.
Kabla ya mtoto huyo kupewa adhabu hiyo Machi 4 kati ya saa 7.45 na saa 8 mchana, wakati mama yake akiwa hayupo nyumbani, inadaiwa mtoto huyo alikuwa aking’ang’ania kula mchana na baba yake. Tabia hiyo ya kung’ang’ania chakula cha baba yake, inadaiwa ilimkasirisha baba huyo akaamua kuchoma moto majani kwa mfano wa mwenge na wakati moto huo ukiwaka, alishika mikono ya mwanawe huyo na kuiweka juu ya moto kwa muda.
Shemeji wa Mnyau, ambaye ni mjomba wa mtoto huyo, Mohamedi Chaurunga, amedai kwamba, baba huyo alipogundua amefanya kosa alijaribu kutoroka katika kijiji hicho ili kukwepa mkono wa sheria.
Chaurunga amedai kuwa, mtuhumiwa alipanga kutoroka baada ya kufahamishwa kwamba taarifa za mtoto wake zimefika kwa mwandishi wa habari ambaye amefika kijijini hapo kuchukua maelezo yake.
“Mnyau ni shemeji yangu na mtoto wake aliyemuunguza amezaa na dada yangu, aliporejea kutoka shambani kwake na kupata taarifa ya kufika mwandishi wa habari kuchukua maelezo ya kijana wake, akajua hana usalama, akaamua kutoroka,” amedai Chaurunga.
Kabla ya kuondoka nyumbani hapo kwenda kusikofahamika, mara baada ya kumpeleka mtoto huyo hospitalini kupatiwa matibabu, inadaiwa kuwa Machi 15 jioni baba huyo alimuaga mkewe na kuondoka zake.
Chaurunga amedai kuwa, baada ya kuarifiwa kuwa shemejiye ana mpango wa kuondoka nyumbani, alishauriwa na wakazi wenziwe wa kijiji hicho cha Nanyanje, wamfuatilie na kumfikisha Polisi.
Mjomba huyo amedai kuwa, aliomba msaada wa vijana wa kijiji hicho wakakubali kufuatana naye na kumkamata.
“Tulipofika kwa mkewe alituambia mumewe ameondoka muda si mrefu, tulimfuatilia njia ya kuelekea kijiji cha Nangaru tukabahatika kumkuta njiani na kumshika na kumpeleka kituo cha Polisi Lindi Mjini,” amesema Mnyau.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Mwakajinga, amethibitisha kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
0 Comments