MWANAMUME anayesadikiwa kuwa jangili, ameuawa kwa kukanyagwakanyagwa na nyati mwenye hasira ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi baada ya kumjeruhi mnyama huyo. Mauaji hayo yaligundulika juzi mchana ambapo inadaiwa kuwa mtu huyo ambaye jina lake halijajulikana mara moja anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 40 na 45, aliingia katika hifadhi hiyo kwa lengo la kuwinda wanyama isivyo halali. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage mwindaji huyo akiwa kwenye harakati za kufanya ujangili hifadhini humo, alishambuliwa na nyati huyo kwa kukanyagwakanyagwa na kuvunjwa mbavu zote.
“Nyati anayedaiwa mwenye hasira baada ya kujeruhiwa, alimshambulia mwindaji huyo haramu na kufa pale pale baada ya mnyama huyo kumvunja mbavu zote kwa kumkanyagakanyaga mwili mzima,” alisema Kamanda Mantage.
Alisema, mwili wa mwindaji huyo, uligunduliwa na askari wa wanyamapori wa hifadhi hiyo waliokuwa doria maeneo hayo kutokana na alama za nyayo za mnyama huyo walizozikuta pembeni ya mwili wa mtu huyo.
“Pia kando ya mwili wa marehemu, askari hao walikuta silaha moja aina ya gobore na risasi zake, mwili huo umehifadhiwa chumba cha maiti katika hospitali ya wilaya mjini Mpanda kwa utambuzi,” alisema Kamanda Mantage.
0 Comments