Mji wa Maswa jana uligeuka uwanja wa mapambano baina ya wananchi na polisi, huku risasi, mabomu ya machozi na mawe vikitumika kama silaha baina ya pande hizo.
Polisi walitumia risasi na mabomu ya machozi kuwadhibiti wananchi waliokuwa wameamua kujichukulia sheria mkononi kumwadhibu mkazi mmoja wa mjini hapa, Masanja Juma (28), aliyetuhumiwa kwa wizi wa kuvunja maduka.
Kutokana na kadhia hiyo, polisi waliamua kutumia risasi za moto ili kuokoa maisha ya mtuhumiwa huyo, lakini wananchi hao nao walikaidi na kuamua kujibu mapigo kwa kuwarushia polisi mawe.
Tukio hilo lililotokea juzi asubuhi lilisababisha shughuli mbalimbali kusimama katika mji wa Maswa.
Kabla polisi hawajatumia nguvu, umati wa wananchi wakiwa na mawe, nondo na mapanga ulimkimbiza Masanja kutoka barabara kuu ya kutoka Bariadi kwenda Maswa, lakini mtuhumiwa huyo alipofika katika jengo la CCM la wilaya aliamua kuingia katika moja ya chumba cha duka linalotumika kuuzia vitabu la ABC Stationery ili kunusuru maisha yake.
Baada ya kujificha, wananchi hao walivamia duka hilo na kuanza kumpiga kwa kutumia mawe na kusababisha uharibifu mkubwa katika duka hilo, hali iliyomlazimisha askari polisi mmoja aliyekuwa lindo katika benki ya NMB tawi la Maswa kufyatua risasi moja hewani.
Kufuatia kitendo hicho, wananchi hao waliokuwa na hasira walianza kumshambulia askari huyo kwa kumrushia mawe, lakini wakati wakiendelea kumshambulia, ghafla liliwasili gari la polisi lenye namba za usajili PT 1890. Hata hivyo, wananchi hao pia walilirushia mawe gari hilo na kuamua kuondoka eneo hilo kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu.
Ilipofika saa saa 4:00 asubuhi walifika askari polisi wanne wakiwa na bunduki aina ya SMG na kuanza kufyatua risasi hewani kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao ndipo mapambano kati ya polisi na wananchi yalianza huku wananchi wakiwashambulia kwa kutumia mawe.
Muda mfupi baadaye, alifika Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Maswa, Benjamin Kuzaga, katika eneo la tukio na kuwasihi wananchi watulie ili polisi wamchukue mtuhumiwa huyo aliyekuwa ndani ya duka hilo, lakini wananchi hao waligoma na kuendelea kuwashambulia askari polisi waliokuwa na silaha kwa mawe.
Ilipofika saa 4:34 asubuhi gari la polisi lenye namba za usajili PT 1890 lilifika tena eneo hilo kwa kasi likiwa na askari polisi waliokuwa wakifyatua mabomu ya machozi na kufanikiwa kuwatawanya wananchi hao na kumpakiza mtuhumiwa kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.
Wakiendelea kufyatua mabomu hayo ili kuwazuia wananchi waliokuwa wakiwakimbilia kwa kuwarushia mawe.
Polisi walimkimbiza mtuhumiwa huyo katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na kipigo.
Umati huo wa wananchi ulihamia katika eneo la hospitali ya wilaya wakipinga mtuhumiwa huyo kupatiwa matibabu, lakini polisi waliimarisha ulinzi na kuwadhibiti.
Katika tukio hilo, askari polisi mmoja mwenye cheo cha Konstebo alipigwa jiwe kichwani, lakini inaelezwa kuwa hali yake inaendelea vizuri. Kabla ya kumshambulia Masanja, wananchi hao walimpiga kwa mawe hadi kumuua Juma Sunge (30), mkazi wa mtaa wa Yasebasi mjini hapa kwa madai ya kuhusika na vitendo vya kuvunja na kuiba kwenye duka linalomilikiwa na Isaya Kidungwa.
Tukio hilo lililotokea Jumamosi iliyopita majira ya saa 8:30 usiku na marehemu kabla ya kufariki dunia alisema kuwa alishirikiana na Masanja kufanya uhalifu huo. Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua wahalifu sambamba na kitendo cha wananchi kuwashambulia askari polisi wanapokuwa wanatimiza wajibu wao.
“Ni vizuri wananchi wakatambua kuwa kujichukulia sheria mikononi ni kosa hivyo ni vema wanapokamata wahalifu wawafikishe katika vyombo vya usalama ili sheria ichukue mkondo wake kwani Mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa hukumu.
0 Comments