Raia wa Pakistan, Nigeria na Afrika Kusini, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kula njama na kusafirisha Gramu 81,000 zenye thamani ya Sh. bilioni 2.8, zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
Washtakiwa hao ni Dennis Okechukwu, Paul Ikechukwu (Nigeria), Stan Hycenth (Afika Kusini) na Shoaib Ayaz (Pakistan).
Walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Mustapha Siani.
Wakili wa Serikali Waandamizi, Biswalo Mganga akisaidiana na Prosper Mwangamila, walidai kuwa kati ya Septemba 26, mwaka jana na Machi 4, mwaka huu, katika nchi hizo, washtakiwa walikula njama ya kusafirisha dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya kuingiza nchini.
Mwangamila alidai Machi 21, mwaka huu katika maeneo ya Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walisafirisha dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya aina ya Heroin za gramu 81,000 zenye thamani ya Sh. 2,835,000,000.
Hata hivyo, kutokana na dawa wanazodaiwa kukutwa nazo kuwa na thamani zaidi ya Sh. milioni 10, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote hadi upelelezi utakapokamilika na kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wakili wa utetezi, Bryson Shayo, aliiomba mahakama kutoa amri ya kuwaruhusu wateja wake kufanya mawasiliano na ndugu zao katika nchi zao, ambao hawana taarifa za kukamatwa kwao.
Wakili Mganga alipinga hoja hiyo na kuhoji kuwa maombi hayo yanafanyika chini ya kifungu gani cha sheria kutokana na kutokuwa na sheria inayotaka vitu vinavyoshikiliwa baada ya washtakiwa kukutwa navyo na Jeshi la Polisi kwa ajili ya upelelezi wa kesi, kurudishwa kwao.
Alidai kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) namba 38 kinaruhusu kitu chochote cha kusaidia upelelezi, ambacho mshtakiwa amekamatwa nacho, wabaki nacho, hivyo kuwapatia simu zao kufanya mawasiliano itakuwa wanaingilia upelelezi wa kesi.
Hakimu Siani alisema mahakama haina uwezo wa kutoa amri yoyote na kuwataka kama wanataka kufanya maombi yoyote wayapeleke Mahakama Kuu. Shauri hilo litatajwa tena Machi 21, mwaka huu.
0 Comments