SERIKALI imesema ipo tayari kulipa kifuta machozi cha Sh. milioni 8.5 kwa kila aliyekufa kwa milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Aidha, wameongezeka watu wawili waliokufa kutokana na milipuko hiyo na sasa idadi kamili kuwa 29.
Kadhalika shule 10 na zahanati zilizoharibika kwa milipuko hiyo, zitaanza kujengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili ziendelee kutoa huduma.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick alisema hayo jana baada ya kupokea misaada kutoka taasisi mbalimbali nchini.
“Tunaomba warithi wa marehemu waharakishe utaratibu wa kupata wasimamizi wa mirathi ili wafungue mirathi mahakamani na hatimaye walipwe kifuta machozi chao,” amesema Sadick.
Amesema fedha hizo ni za Serikali na wala hazitokani na michango ya wahisani waliokuwa wakitoa misaada kwa waathirika.
Kuhusu idadi ya waliokufa, alisema walioongezeka wawili, mmoja aliaga dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kuhusu ujenzi wa shule na zahanati 10 zilizoharibiwa, alisema ujenzi utaanza mara moja kwa kuwa huduma zinahitajika kuendelea katika maeneo hayo na jana Shirika la JKT la Suma JKT lilikuwa likifanya tathmini ya kuona unahitajika ujenzi wa aina gani.
Amesema, shule tatu kati ya 10 zimepata wahisani wa kuzijenga upya ambazo ni sekondari ya Pugu itakayojengwa na Taasisi ya Shree Hindu Mandal, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliyokubali kujenga shule moja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga shule moja na saba zilizobaki zitajengwa na Suma JKT haraka.
Katika hatua nyingine, wakazi wa Mazizini ambao walikuwa wakilalamika kuathiriwa na mabomu na kukohoa, kuumwa kifua na kuharisha, Serikali imesema itawasiliana na JWTZ na Wizara ya Afya ili iwapime afya zao kwa umakini zaidi.
0 Comments