Wakati maelfu ya watu wakizidi kumiminika katika kijiji cha Samunge, kata ya Digodigo Wilaya ya Ngorongoro kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile kupata tiba, Serikali imesitisha safari hizo kwa wiki moja kutokana na mrundikano mkubwa wa watu na magari.Mkuu wa Wilaya alisema kuongezeka kwa watu kunatokana na uongo unaonezwa na baadhi ya watu kwamba Mchungaji Mwasapile atafunga huduma yake kwa ajili ya Kwaresima inayoanza kesho.
Kuna taarifa kutoka baadhi ya hospitali kwamba baadhi ya ndugu za wagonjwa wa wenye virusi vya Ukimwi, saratani, kisukari na pumu waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini wameanza kuwaondoa wagonjwa wao na kuwapeleka kwa mchungaji huyo.
Wananchi hao ambao wametoka katika mikoa mbalimbali na nchi jirani za Kenya na Uganda, wamemiminika katika kijiji hicho wakitaka kupatiwa tiba kutoka kwa Mchungaji Mwasapile.
Wengine waliofika na kupata huduma, wanashindwa kurudi makwao kutokana na kukosa usafiri kwa kuwa magari yanayowapeleka huondoka kabla hawajapata huduma.
WATU SABA WADAIWA KUFARIKI DUNIA
Pia, msongamano huo wa watu umesababisha vifo vya baadhi ya watu waliopelekwa wakiwa mahututi kutokana na kuchelewa kupata huduma.
Hadi kufikia juzi, watu saba walikuwa wamefariki dunia akiwemo mtoto mmoja.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia maiti hizo na wagonjwa wengine waliofikishwa wakiwa na dripu mikononi na wengine wakiwa hawajiwezi kabisa.
Pamoja ya kuwa mchungaji Mwasapile alijitahidi mno kuwahudumia wagonjwa ambao walifika sehemu hiyo, lakini ilipofika juzi jioni ilibidi waongeze wachungaji wengine wawili kumsaidia ili kupunguza msongamano wa watu kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wagonjwa wanavyozidi kumiminika.