Baraza la Umoja wa Mataifa limeiondoa Libya kama mwanachama wa tume ya haki za binadamu.
Uwamuzi huo wa pamoja unazidi kumtenga zaidi kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.Hatua hii inafuatia tangazo la kumuekea Kanali Gaddafi, familia na washirika wake vikwazo kutoka kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na Muungano wa Ulaya.
Utawala wa Libya umelaaniwa vikali kwa
kundelea kuwadhulumu raia wake wanaoandamana dhidi ya serikali.
Wakati huo huo mapigano nchini Libya yamepelekea raia wa taifa hilo kutorokea mataifa jirani ya Tunisia na Misri. Maaifisa wa Umoja wa Mataifa wamesema zaidi ya watu 140,000 tayari ni wakimbizi katika mataifa hayo mawili, huku wengine wengi wakiwa mpakani.
Hali hii inaripotiwa kuzoroteshwa zaidi na hali ya usalama duni magharibi mwa Libya ambayo imeifanya vigumu kwa msaada wowote kutolewa kwa waathirika wa mapigano hayo.
Inadaiwa Majeruhi wanauawa katika mahospitali na wakati wakiwa kwenye magari ya kusafirisha wagonjwa.
Serekali ya Italy imeahidi kutuma msaada wa dharura katika mpaka wa Libya na Tunisia kutoa msaada kwa wakimbizi ambao wanahitaji malazi, chakula, maji na huduma za matibabu.
Licha ya hayo kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi amesimama kidete akisema hakuna kitakachomshawishi kungatuka mamlakani, huku akiendelea kulaumu mataifa ya magharibi pamoja na mtandao wa Al - Qaeda kwa kusababisha msukosuko wa kisiasa nchini humo.
0 Comments