Alisema hayo katika ibada na sherehe za kumsimika na kumweka wakfu Askofu wa jimbo Katoliki Dodoma, Gervas Nyaisonga, iliyofanyika katika viwanja vya kanisa kuu la Mt. Paulo wa Msalaba mjini hapa.
“Msisite kuwakemea wanasiasa wanaotaka kupotosha amani kwa misingi ya itikadi zao za kisiasa na kuvuruga tunu tulizonazo… tukiipoteza hali ya amani na utulivu uliopo sasa tutakosa muda wa kuirejesha hata muda wa kujiletea maendeleo,” alisema.
Alisema viongozi hao wana nafasi kubwa ya kuwaeleza viongozi wa kisiasa kujifunza kuvumiliana.
Pia alisema tofauti za kisiasa na kimtazamo haziwezi kuepukika lakini jambo la muhimu ambalo linaweza kulinda amani na utulivu ni kuvumiliana.
“Wahimizwe Watanzania kuvumiliana pamoja na wanasiasa bila kujali tofauti zetu za kisiasa, lakini ya msingi yanayotuunganisha wote ni ubinadamu wetu, hakuna mtu mwenye haki zaidi ya mwenzake,”alisema.
Aliwasisitiza viongozi wa dini kupitia madhehebu yao, kuwalea kiroho na kuhakikisha kuwa wanahimiza amani, utulivu na ustawi wa maadili bora nchini.
Kikwete alisema wao ni kati ya watu ambao jamii imekuwa ikiwaamini na kuvuta usikivu mkubwa kwao hivyo ni vema wakahubiri amani, upendo, mshikamano na kujenga maadili mema kwa kila Mtanzania.
Aliwataka viongozi hao kutochoka kuhubiri amani na utulivu na kuwataka watu wapendane pasipo kujali dini, kabila wala itikadi za kisiasa.
Akizungumzia suala la elimu, alisema madhehebu ya dini yamekuwa yakisaidiana na serikali kwa namna mbalimbali katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo elimu.
Alisema kutokana na ushirikiano huo serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika vyuo vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini kwani mpango huo awali ulikuwa kwa vyuo vinavyomilikiwa na serikali.
Aidha, aliyaomba madhehebu ya dini na taasisi mbalimbali kuelekeza uwekezaji wao katika kutanua ongezeko la nafasi za kidato cha tano na sita kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa.
Alisema serikali pekee haiwezi haiwezi kuongeza nafasi za wanafunzi wa kidato cha tano na sita, ingawa mpango huo upo kwa sababu mahitaji ni makubwa sana.
Rais Kikwete alisema hata kama serikali itaamua kupunguza shule za kidato cha kwanza hadi cha nne, haitaweza kukabiliana na mahitaji hayo.
Naye Mhadhama Kardinali Polcarpy Pengo, alimtaka askofu huyo mpya kuliongoza jimbo la Dodoma kwa kuliweka katika misingi ya Mungu na kutoliweka jimbo hilo rehani kwa matajiri kwa kuahidiwa fedha nyingi.
“Uaskofu unapaswa kutumikia na wala si kutawala na kuhimiza waumini kushirikiana nawe,”alisema na kuongeza:
“Kazi yako ni kutenda lile ambalo Mungu amekuagiza utende…Yeyote anayefanya utume wa kazi ya kiaskofu akitaka kujilinganisha na mtu mwingine anajitafutia shida na kifo,”alisema.
Kwa upande wake, Rais Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Askofu Yuda Ruwaichi, aliwataka viongozi wa dini kuwa na mshikamano na kutoruhusu chembe za kuwagawa ziote mizizi.
“Mjenge umoja, upendo, amani na mshikamano usijali itikadi za kisiasa, kikabila, kidini na hata mpasuko wa matajiri na masikini,” alisema.
Licha ya sherehe hizo kutawaliwa na mvua iliyokuwa ikinyesha mjini hapa, maaskofu wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi waliandamana hadi katika jukwaa liloandaliwa kwa ajili ya sherehe hizo.
Katika sherehe hizo, Askofu Nyaisonga alikabidhiwa magari mawili na fedha taslimu zaidi ya sh. milioni 10 kutoka katika majimbo mbalimbali aliyowahi kuyatumikia akiwa padri.
Viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Mama Anne Mkapa.
0 Comments