WATUHUMIWA watano wa ujambazi kati ya 10 walioua polisi wawili wakiwa mahabusu wameuawa.
Wananchi wenye hasira wamewaua watu hao katika maeneo tofauti , Jeshi la Polisi limemkamata mtuhumiwa mmoja.
Askari Polisi waliouawa walikuwa katika Kituo Kidogo cha Kagongwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga, majambazi wengine wanne wakiendelea kusakwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, ameyasema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Jeshi lake la kuwatafuta watuhumiwa hao 10 waliotoroka na silaha baada ya kufanya mauaji katika kituo hicho cha Polisi.
Watuhumiwa hao ni Kwizela Lionel (26), mfanyabiashara mkazi wa Bujumbura nchini Burundi, Ilokoze Willy (39) au maarufu Karumanzira, dereva mkazi wa Bujumbura, Simon Mathias au Fred Setty (27), dereva pikipiki mwenye makazi Isamilo jijini Mwanza, Mwenge jijini Dar es Salaam na Moshi mkoani Kilimanjaro na Paulo Gilioma au Babu (40) mkazi wa Nyasubi wilayani hapa.
Kamanda huyo alisema, katika msako ulifanyika katika vijiji vya Iponya, Kishima, Igusule, Motange na Mwalugulu, Machi 16, mwaka huu saa tatu usiku, wananchi walitoa taarifa Polisi kuwa kuna watu watatu waliokuwa wamejificha katika msitu wa Igusule.
Iligundulika kuwa alikuwa amejificha jambazi Selemani Mposi, wengine Kennedy William, Goodluck Leonard au Papaa walikuwa wamejificha katika sehemu nyingine.
Alisema, baada ya wananchi kuwaona, walitoa taarifa Polisi, ndipo Polisi walipofika sehemu hiyo ili walitaka kumkamata Mposi, lakini alianza kukimbia baada ya Polisi kufika na hivyo kumfyatulia risasi katika sehemu ya mguuni; hivyo kushindwa kukimbia na kukamatwa.
Alisema, baada ya kumkamata, walimhoji mtuhumiwa huku akiwa anavuja damu nyingi na alifariki dunia wakati akifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu huku wakiamini angeendelea kuwa hai; hali ambayo ingefanya Polisi kupata taarifa zaidi za wengine waliohusika katika tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema msako uliendelea kufanyika hasa katika msitu huo ambako jambazi mwingine, John Peter ‘Ngosha’ alikamatwa katika Kijiji cha Usule huku akiwa dhaifu baada ya kukosa chakula.
Wananchi walitoa taarifa Polisi na kufika katika eneo hilo na kumdhibiti hadi kumfikisha hospitalini. Hata hivyo, mtuhumiwa huyo naye alifariki dunia saa 9.30 alasiri.
Aidha, Emmanuel Jackson naye alikamatwa katika maeneo hayo huku jitihada za wananchi kusaidiana Polisi zilizaa matunda baada ya kumkurupusha mtuhumiwa huyo katika msitu huo.
Kamanda Athumani alisema Jackson anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi huku akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi ili kuwakamata watuhumiwa wengine waliotoroka na silaha baada ya mauaji ya askari Konstebo Salimu Mwanakatwe na Konstebo Ndira Ngwegwe.
Marehemu Mwanakatwe alipelekwa Kahama kwa ajili ya kazi maalumu iliyokuwa ikifanywa na kikosikazi cha Jeshi hilo.
Habari za uhakika zilisema marehemu huyo kabla ya mauti alikuwa dereva wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, na pia ni mtoto wa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka cha Tanzania (FAT), Ally Mwanakatwe.
0 Comments