Aliyekuwa Mshauri wa Rais Zanzibar, Mohammed Raza, amesema asiyetaka Muungano sio mwana halali wa Zanzibar, kwa vile umesaidia kujenga umoja wa kitaifa na udugu kati ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, mjini Zanzibar jana. “Asiyetaka Muungano sio mwana halali. Na bahati mbaya wanaokataa Muungano hawafahamu faida ya kuwa na umoja,” alisema Raza.
Hata hivyo, alisema Zanzibar kama mdau mkuu wa Muungano, ni vizuri muswada wa kuweka utaratibu wa marekebisho ya Katiba ukapitishwa na wabunge kwa kuzingatia theluthi mbili ya wabunge kutoka kila upande wa Muungano.
Aliwataka wabunge wa Zanzibar kutokubali muswada huo kupitishwa kwa wingi wa kura za wabunge, kwa vile wabunge wa Zanzibar ni wachache ukilinganisha na wa Tanzania Bara.
Aidha, aliwataka Wazanzibari kujenga hoja wakati wa mjadala wa Katiba mpya utakapofika na kuondoa woga na kuwa wakweli katika kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. “Wakati wa kuzungumza maslahi ya nchi mbili tuzungumze hoja na tuondoe woga na tuwe wakweli.
Zanzibar tunapenda Muungano. Tusitukane. Tuondoe jazba,” alisema.
Aliwataka viongozi wa dini kufanya kazi ya kuwaombea dua watendaji ili watayarishe muswada mzuri, utakaoleta maslahi ya pande zote mbili za Muungano.
Hata hivyo, alisema matatizo yaliyofikia Zanzibar katika Muungano, yamesababishwa na unafiki wa watendaji ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba (SMZ).
“Matatizo yaliyotufika Zanzibar yanatokana na unafiki wa sisi Wazanzibari. Tusiwabebeshe mzigo wa lawama wenzetu wa Tanzania Bara na kukwepa udhaifu wetu,” alisema Raza.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments