Rais wa Ivory Coast anayetambulika na jamii ya kimataifa, Alassane Ouattara, ametoa wito wa kuwepo kwa hali ya utulivu baada ya kumkamata mpinzani wake Laurent Gbagbo.
Akitangaza kuanza kwa uchunguzi juu ya Bwana Gbagbo,alimuahidi kuwa atapata haki zake na kwamba tume ya haki na maridhiano itaanzishwa.
Bwana Gbagbo alijisalimisha baada ya mashambulio ya kijeshi katika nyumba yake mjini Abidjan.
Alichochea mapigano hayo kwa kukataa kuondoka madarakani,huku akisisitiza kuwa ameshinda uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba mwaka uliopita.
Lakini majeshi yanayomuunga mkono Ouattara yakavamia makaazi yake siku ya Jumatatu, huku vifaru vya Ufaransa vinavyosaidia vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa vikiwa karibu.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameridhishwa na hatua ya kukamatwa kwa Bwana Gbagbo,akisema hatua hio imemaliza mapigano ambayo hayakuwa na msingi,na kwamba umoja wa mataifa utaunga mkono serikali mpya.
Rais wa Marekani Barack Obama pia aliridhishwa na kukamatwa kwake, na kutoa wito kwa makundi yenye silaha nchini Ivory Coast kuzisalimisha ili kutoa fursa ya kujenga mfumo wa demokrasia.
0 Comments