KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa amemsimamisha kazi Katibu wa Wilaya ya Nzega wa chama hicho, Sunny Yohana.
Dk. Slaa ambaye yupo mkoani Tabora akiendelea na ziara yake ya kikazi ya chama hicho akianzia Tabora Mjini, Bukene, Nzega na leo atahutubia wananchi wa Igunga na kuendelea na wilaya zilizosalia mkoani hapa.
Alisema amefikia uamuzi huo wa kumsimamisha kazi Katibu huyo wa Wilaya baada ya kupokea malalamiko mengi ya utendaji kazi wake katika kikao cha wanachama kilichofanyika jana katika Ukumbi wa Channel One ambacho kilikuwa kama hukumu ya katibu huyo.
Mambo ambayo yalichangia kuenguliwa kwa muda katika kiti hicho ni pamoja na kutokuwa na ushirikiano na Umoja wa Vijana na baadhi ya wanachama ambao walikuwa wakimshutumu kwa kuwa na ubinafisi.
Wanachama hao walidai mbele ya Dk. Slaa kuwa katibu huyo amekuwa akiukataza umoja wa vijana kufanya mikutano ya ndani na hata ile ya nje, jambo lililomshangaza Katibu huyo Mkuu wa Taifa.
Wakiendelea kubainisha wanachama hao juu ya utawala wa Yohana, walidai alithubutu hata kusimamisha michango ambayo ilikuwa akitolewa na wanachama hao ili kupata mfuko wa chama hicho.
Hata hivyo, chama hicho kwa sasa hakina hata akaunti ya kutunzia fedha.
Pamoja na hayo, jambo ambalo lililochangia kwa kiasi kikubwa kumsimamisha katibu huyo ni pale aliwasilisha hati ya bajeti ambayo iligharimu maandalizi ya ujio wa msafara wa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kwa upande, Yohana alisema ameyapokea vizuri maamuzi hayo ya Katibu Mkuu kuwa ili chama kiendelee mambo kama hayo hutokea kuwajibishana na kwamba ataendelea kuwa na mapenzi na chama hicho.
Alisema kwa tamko hilo ingawa hakupewa hata muda kidogo wa kujitetea juu ya tuhuma hizo, aliuangushia mzigo kwa umoja wa vijana kumuundia njama za kumtengua cheo hicho.
Dk. Slaa alimteua Peter Pius kuwa Kaimu Katibu wa Chadema Wilaya mpaka Tume maalumu itakapofanya uchunguzi, huku akitoa mwito kwa wanachama kushirikiana na kuacha kukigawa chama hicho.
0 Comments