KLABU Bingwa ya Afrika, timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imekumbwa na kashfa baada ya waamuzi waliochezesha mechi yao na Simba kudai mabingwa hao walitaka kuwahonga. (Pichani shabiki wa Tp Mazembe akiongea na Azim Dewji na kujitapa juu ya ushindi)
Mchezo huo wa kwanza wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika ulifanyika mjini Lubumbashi, DRC wiki mbili zilizopita na TP Mazembe kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Timu hizo mbili kesho zinarudiana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo ili isonge mbele Simba inahitaji ushindi wa mabao 2-0, hivyo itakuwa imeivua ubingwa Mazembe ambayo Desemba mwaka jana ilifika fainali ya klabu bingwa ya dunia na kufungwa mabao 3-0 na klabu bingwa ya Ulaya, Inter Milan.
Kulingana na taarifa zilizopatikana jana kwenye mtandao wa ahram.org.eg wa nchini Misri, ulieleza kuwa maofisa wa Shirikisho la soka la Afrika (Caf) wamethibitisha kuwa waamuzi wanne kutoka nchini Misri waliripoti kuwa TP Mazembe iliwatishia maisha baada ya kukataa kupokea rushwa ya dola 10,000 za Marekani ili waisaidie ishinde dhidi ya Simba.
“Waamuzi hao Yasser Abdel-Raouf, Ayman Deguesh, Tamer Salah na Fahim Omar waliwasilisha ripoti yao Caf ikilieleza Shirikisho hilo kuwa walipewa ofa ya rushwa ya dola za Marekani 10,000 ili kurahisisha kazi ya kupata ushindi kwa TP Mazembe ilipokumbana na Simba,” Ofisa wa CAF aliuambia mtandao huo.
Mtandao huo unaeleza zaidi kwamba hali ilikuwa mbaya kwa waamuzi hao baada ya kukataa kupokea rushwa kabla ya mchezo huo, hivyo kutishiwa maisha, endapo wangeripoti jambo hilo.
Kwa mujibu wa mtandao huo waamuzi hao walishindwa kutangaza jambo hilo hadi waliporejea kwao Cairo, Misri. Makao Makuu ya Caf yapo Cairo.
Licha ya mtandao huo wa Misri, lakini juzi na jana mitandao mbalimbali ya intaneti kulikuwa na mijadala kuhusiana na taarifa hizo, ambapo mtandao uitwao discussion.ghanaweb.com nao ulikuwa na taarifa hizo, huku baadhi ya wadau wa soka wakitoa maoni kwamba TP Mazembe ilikuwa haihitaji kutoa fedha kwa sababu ya kuishinda Simba, hivyo taarifa hizo si za kweli.
Wakati huohuo, akizungumza mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema ameshtushwa na taarifa za kwenye mtandao kuhusiana na Mazembe kudaiwa ilitaka kuhonga waamuzi wa mechi yao.
“Nilipogundua hili, haraka sana nikaanza kulifuatilia kwa karibu, maana mwanzo nilijua ni mambo ya Siku ya Wajinga Duniani, lakini kuangalia vizuri taarifa iliwekwa Machi 30, hivyo nikaamua kuchukua hatua.
“Tumeshaandika barua TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), maana ndiyo yenye mamlaka ya kuwasiliana na Caf (Shirikisho la Soka Afrika), kuwaambia tunacheza Jumapili (kesho) lakini tukiwa na pingamizi kuhusiana na jambo hili.
“Ni vyema sheria za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kanuni ya 24 inayozungumzia mambo ya rushwa ikafuatwa kumaliza jambo hili,” alisema Rage.
Kulingana na mtandao wa Caf Kanuni hiyo ya 24 inaeleza kuwa: “Ikitokea ndani ya miezi mitatu kufuatia kila mechi iliyochezwa ndani ya muundo wa michuano hii, Caf ikitaarifiwa, bila ya kujali chanzo cha habari hiyo ni kipi, kuwepo kwa uvunjifu wa sheria na udanganyifu katika mchezo kulikofanywa na mojawapo ya timu, utafanyika uchunguzi mara moja juu ya suala hilo na endapo suala hilo litathibitika hatua zifuatazo zitachukuliwa.”
Inafafanua hatua hizo kuwa ni 1: Endapo kosa limefanywa katika raundi ya awali ya michuano na kugundulika kabla ya kuanza kwa raundi inayofuata, timu ya mwisho ambayo ilikuwa ya mwisho kuondolewa kwenye michuano na timu husika itarejeshwa kuendelea na michuano hiyo katika raundi hiyo.
Na timu iliyopatwa na hatia itafungiwa kushiriki kwenye mashindano yote yanayosimamiwa na CAF kwa miaka miwili.
2 : Endapo makosa yatagundulika baada ya kuanza kwa raundi nyingine inayofuata ya michuano hiyo, timu iliyopatikana na hatia itaondolewa kwenye michuano hiyo na timu ambayo itakuwa mpinzani wake wa mwisho itapewa nafasi yake na pia itafungiwa kucheza michuano yote ya Caf kwa kipindi cha miaka mitatu.
3: Endapo litakuwa limefanyika wakati wa mechi ya fainali na klabu ambayo itakuwa imetwaa ubingwa, klabu hiyo itatakiwa kurudisha kombe ambalo litakabidhiwa kwa mshindi wa pili na timu iliyopatikana na hatia itafungiwa kwa miaka mitatu kushiriki katika michuano yote ya CAF.
4 : Endapo itabainika chama cha soka ambacho timu iliyopatikana na makosa inatoka ilishiriki kuisaidia klabu hiyo kutenda kosa hilo, chama hicho na klabu zote ambazo ziko chini ya mamlaka yake zitafungiwa kushiriki kwenye michuano ya CAF ya klabu kwa kipindi cha miaka mitatu.
5: Kesi iliyotajwa katika kifungu hiki italazimika kuamuliwa na Kamati ya Mashindano ya Caf. Wakati huohuo, Betram Lengama anaripoti kuwa mashabiki TP Mazembe waliowasili jana jijini Dar es Salaam wamejigamba timu yao itaibuka na ushindi kesho.
Mmoja wa mashabiki hao Serge Nkunde alijigamba baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kuwa watainyuka Simba mabao 3-0 na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Alisema watatoa kipigo hicho alichokiita kidogo kwa sababu Tanzania ni rafiki mkubwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nkunde ambaye aliwaambia waandishi wa habari uwanjani hapo kwa ajili ya kushuhudia ujio wa TP Mazembe, lakini badala yake kuambulia kuwasili kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuwa ushindi ni lazima japokuwa watakuwa na huruma kiasi kwa Watanzania.
“Ushindi wa mabao 3-0 ni lazima na tutawafunga mabao hayo kwa sababu tu Watanzania ni marafiki zetu wakubwa hatuwezi kuwadhalilisha kwa kuwapa kipigo kikubwa,” alijinasibu Nkunde.
Nkunde aliyekuwa akiongea kwa kujiamini, alisema TP Mazembe kama mabingwa wa Afrika haiogopi timu yoyote na wanaweza kwenda popote bila wasiwasi kutokana na ufalme huo.
Majibu hayo yalitokana na waandishi kumuuliza sababu ya Mazembe kuhofia kutaja muda na ndege sahihi watakayokuja nayo.
Hata hivyo Nkunde alisema wao wamepanga kufunga mabao 3-0, lakini kama Simba wataleta ‘nyodo’ katika mchezo huo watakumbana na kipigo kikali cha mabao 8-0 .
0 Comments