UTOAJI maoni juu ya uundwaji tume ya kuendesha mchakato wa Katiba mpya nchini umeingia dosari kwa mikutano ya Dodoma na Dar es Salaam kugubikwa na vurugu.
Katika mikutano yote ya jana, polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kutuliza ghasia, huku
Dodoma wakitumia risasi na mabomu ya kutoa machozi kutawanya kundi la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) alikiri jana kusababisha vurugu za Dodoma katika eneo la ukumbi wa zamani wa Bunge wa Pius Msekwa mjini hapa. Mbunge huyo alikiri jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk
James Msekela kuhamasisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwenda kwenye ukumbi huo kutoa maoni ya Katiba na kusababisha vurugu kubwa, iliyolaz-imu polisi kufyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi nje ya jengo hilo.

Lema alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya Msekela kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu vurugu hizo na kueleza kuwa zilisababishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa
wanaotumia vijana kuvuruga amani ya nchi na kwamba alipata taarifa ya kuwapo wanasiasa waliokwenda Udom kuhamasisha wanafunzi kuja bungeni Alhamisi.

Baada ya kauli ya Msekela iliyoambatana na kupiga marufuku wanasiasa kufanya kampeni Udom kwa kuwa ni kinyume cha sheria, Lema alijitokeza papo hapo na kukiri kuwa yeye ndiye aliyekwenda Udom na alizungumza na wanafunzi nje ya chuo kwa mujibu wa sheria na hakuwahamasisha kurusha mawe.

“ Jumamosi hii nakwenda tena, ni wajibu wangu nikiwa mbunge kufanya hayo, nisingependa kutishwa kabisa, huo ni wajibu wangu mbunge kuhakikisha watu wanauelewa muswada, napenda Mkuu wa Mkoa uelewe kuwa mimi nilikwenda na nitakwenda tena kufungua tawi la chama Jumamosi hii, sheria inaniruhusu,” alisema Lema ambaye baadaye aliwaambia waandishi kuwa atakwenda na Mkuu huyo akitaka kumkamata, amsubiri huko na haogopi, maana sheria anazijua.

Lema alisema alikwenda kuhamasisha wasomi waje kutoa maoni kuhusu Katiba kwa kuwa
wauza nyanya na wafanyabiashara wa magengeni, hawawezi kutoa maoni kwa sababu hawaelewi Kiingereza na masuala ya Katiba, ila wasomi.

Katika eneo la Bunge, watu waliodhaniwa kuwa wananchi, lakini asilimia kubwa kujulikana kuwa ni wanafunzi wa Udom, walizuia njia huku wakiimba nyimbo za kudai Katiba mpya kwa uhuru, lakini baadaye vurugu zilipozidi, Lema aliyekuwa ndani ya ukumbi wa maoni, alitoka nje na kuwataka watu hao watulie ili utaratibu wa kwenda uwanja wa Jamhuri zifanyike, lakini walisikika wakisema, “Lema umetusaliti.”

Baadhi yao, walifika eneo la Bunge mapema asubuhi na kulazimisha kuingia ukumbini bila kupekuliwa, tena kwa idadi kubwa, huku ukumbi huo ukiwa na uwezo wa watu 540 na walipoelezwa kusubiri utaratibu wa Kamati kwenda kupokea maoni yao ukumbi wa Chimwaga (Udom), walianza kurusha mawe na kusababisha Mkuu wa Mkoa kuamuru polisi waingie
kazini.

Hali ya tafrani iliyozuka katika milango ya kuingilia eneo la Bunge kuanzia asubuhi, ilisababisha Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) kutanda katika maeneo hayo, huku mchakato
wa kupokea maoni kwa wananchi walioingia ukumbini ukiwa unaendelea, lakini vurugu
zilipozidi, FFU wakiwa na gari lao waliingia kutoka nje ya uzio wa Bunge kwa kasi na kufyatua risasi walikokuwa wananchi na wanafunzi hao.

Hata hivyo, Msekela alisema uongozi wa Bunge umekubali kwenda Chimwaga saa 10 jioni Alhamisi ili kupokea maoni ya wanafunzi hao kuhusu Mchakato wa Muswada wa Uundwaji wa Tume ya kukusanya maoni ya uanzishwaji wa Katiba Mpya, lakini kinachotokea ni kutoelewa kwa wanafunzi kuwa si kupokea Muswada wa Katiba Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Bunge kuhusu tukio hilo, Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashililah, alisema tukio hilo ni la aibu na waliofanya fujo hawakutumia busara wala hekima, kwa kuwa uwezo wa ukumbi ni mdogo na kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Bora iliyopo hapa ilisharidhia kwenda Chimwaga.

“Ukumbi ni mdogo, tunapata shida, ni kwa namna gani mtu kama ana nia njema ya kutoa maoni anakuja na mawe mfukoni, maoni gani yanatolewa kwa mawe, si busara, tuliliona hilo la ukumbi na tukakubaliana awamu mbili za kupokea maoni, asubuhi mpaka saa nane na saa tisa kuendelea, tulipobaini wengi ni wanafunzi, tukasema kamati iende Chimwaga, lakini hawataki,” alisema Dk. Kashililah.

Polisi walipoanza kufyatua risasi zaidi ya milio 20 ilisikika huku mabomu ya kutoa machozi
nayo yakifuatia na kusababisha wanafunzi na maelfu ya watu waliokuwa nje ya jengo la Bunge
kukimbia bila mpangilio na kusababisha kamera za wapiga picha kuharibika, watu kuanguka na
wengine kupigwa mawe. Hata hivyo, hakuna taarifa za waliojeruhiwa kiasi cha kukimbizwa hospitalini kwa kuwa Polisi ilirejesha amani baada ya tafrani hiyo.

Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti nje ya jengo la Bunge, wanafunzi wa Udom walisema
hawataki kwenda Chimwaga kwa kuwa wanahisi ni ujanja wa kisiasa kwani walipata matangazo
yakiwataka waje Msekwa na si Chimwaga na kama Kamati inataka waende Chimwaga, basi waambatane.

“Hakuna anayeondoka hapa, tunataka twende Jamhuri ili kila mtu aseme, kama hawataki nasi hatuondoki hapa, kama ni Chimwaga twende mguu kwa mguu,” alisema Petro Karungamya, na kuungwa mkono na mwanafunzi mwenzake, Haruna Mikidadi. Kamati hiyo ndogo ya kupokea
maoni Dodoma ilikuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala Bora, Angela Kairuki.

Kamati nyingine mbili ziko Dar es Salaam na Zanzibar na zitakusanya maoni kwa siku tatu, Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi na ikibidi Jumapili. Naye Halima Mlacha anaripoti kuwa mkutano wa Dar es Salaam wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Uundwaji Tume ya Mapitio ya Mabadiliko ya Katiba ya nchi wa mwaka 2011, ulivurugika na kulazimika kusitishwa hadi leo kutokana na kuzuka vurugu na mapigano wakati mkutano huo ukiendelea.

Vurugu hizo zilianza baada ya Naibu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda CCM, Tambwe Hizza, kutoa maoni kwa niaba ya chama hicho, na kujikuta akizomewa na kuitwa fisadi mara alipoanza kusifia jitihada za Serikali za kuanzisha mchakato huo wa kuunda Katiba mpya.

“Muswada huu ni jitihada za Serikali za kuwasikiliza wananchi, yatakayoongelewa yatazingatiwa, lakini pia mikutano hii ya hadhara isitumike kumnyima Rais madaraka
yake,” alisema Tambwe na kabla ya kumalizia hoja yake alizomea na vurugu kuibuka.

Gazeti hili lilishuhudia ukumbi wa Karimjee ambako mkutano huo ulikuwa ukifanyika ukichafuka ghafla, kwa washiriki, wengi wao wakiwa vijana, kutishia kumtoa mbele Tambwe huku waliokuwa wakimtetea, wakiambulia kupigwa nao bila kukubali na hivyo kuzuka
mapigano.

Hata hivyo, polisi waliokuwa eneo hilo na wengine kuongezeka walidhibiti tafrani hiyo ingawa mkutano huo ulishindwa kuendelea kutokana na Tambwe kugoma kukaa chini na badala yake kuimbwa kwa kebehi.

“Aondoke, CCM ni aibu, fisadi,” ndiyo maneno ya nyimbo yaliyokuwa yakisika ukumbini hapo huku baadhi ya waliohudhuria wakishindwa kuvumilia na kuvamia eneo alilosimama Tambwe hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na mkutano huo kusitishwa.

“Kamati ilikuja hapa kukusanya maoni ya wananchi juu ya muswada huu, lakini wote ni mashahidi wa mazingira yaliyojitokeza muda mfupi, hivyo Kamati imeridhia kusitisha
mkutano huu hadi kesho (leo) ili kutengeneza mazingira mazuri ya kukusanya maoni haya,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Gosbert Blandes.

Awali akiwasilisha maoni yake mbele ya baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba, alisifu juhudi za Rais Jakaya Kikwete za kutengeneza muswada huo, lakini pia alishauri wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni juu ya masuala muhimu
yanayowahusu na kipengele kinachowabana kirekebishwe.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe, alionesha kusikitishwa na vurugu zilizotokea na kusisitiza kuwa mkutano huo lengo lake ni kupokea maoni ya mwananchi yeyote yawe mabaya au mazuri na kuyafanyia kazi yatakayoonekana kuwa na tija kwa Watanzania.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alitaja baadhi ya vifungu katika muswada huo virekebishwe likiwamo suala la kupewa madaraka makubwa Rais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupewa jukumu la kusimamia utaratibu wa kupigia kura Katiba hiyo.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema shinikizo na hamasa la kuundwa kwa Katiba mpya lilitoka kwa vyama vya upinzani, lakini kwa bahati mbaya muswada huo haujavitaja vyama hivyo.

James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alipendekeza muswada huo upelekwe bungeni na Ibara ya 98 ya Katiba ibadilishwe, ili kuwezesha kuundwa Baraza la Kutunga Katiba, ambalo litasimamia uteuzi wa makamishna wake na sekretarieti, kuliko
kumwachia kazi hiyo Rais pekee kama muswada unavyosema.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, alisema kitendo cha baadhi ya washiriki katika mkutano huo kuanzisha vurugu ni cha kusikitisha, kwa kuwa kinawanyima wananchi wengine fursa na uhuru wa kutoa maoni yao juu ya muswada huo.

Wakati huo huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani amesema mchakato wa kupokea maoni ya uundwaji wa Katiba Mpya utaigharimu Serikali zaidi ya Sh bilioni 27 kwa sasa na kiwango hicho kinaweza kubadilika kulingana na mahitaji ya mchakato.

Aidha, amelaani upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu hasa wanasiasa kuwa kinachofanyika Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar siku hizi nne ni utoaji maoni ya
wadau kuhusu Muswada wa Katiba Mpya, kitu ambacho si kweli kwa kuwa ni maoni ya Muswada wa Uundwaji wa Tume itakayopokea maoni ya wananchi.

Waziri aliwaondoa hofu wananchi na wadau wote kuhusu suala hilo kwa kusema Bunge limeongeza Jumapili pia itumike itakapobidi na kwamba Serikali itazingatia na kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) na wananchi wengine kuhusu Tume hiyo kwa kuwa serikali ni sikivu wakati wote.

Kombani alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha mwaka 2014 Katiba Mpya inapatikana na Muswada wa Uundwaji wa Tume, baada ya maoni, utafikishwa bungeni Aprili 18 ili upitishwe
na ipatikane sheria itakayowezesha Tume kuanza kazi Juni mosi.