Raia wanne wa Kenya wanaodai kuwa walinyanyaswa wakati kundi la Mau Mau lilipokuwa likikandamizwa na utawala wa Mkoloni wameanzisha kesi dhidi ya serikali ya Uingereza.
Kundi hilo linalodai fidia kupitia Mahakama kuu, linasema kuwa walishambuliwa kati ya mwaka 1952 na 1961 na maofisa wa utawala wa mkoloni Uingereza.Wakili wa watu hao Martyn Day anasema kuwa, "mateso yaliyowafika yaliwaacha wakiwa na madhara ya kudumu maisha yao yote,"
Serikali inasema kuwa tangu mateso yanayodaiwa kufanyiwa watu hao ni muda mrefu. Kwa hiyo haiwezi kuwajibishwa.
Kesi hii imewasilishwa na wanaume watatu na mwanamke mmoja, wote wakiwa na umri uliozidi miaka 70.
Wakili wao anasema kuwa watu hawa wanawakilisha jamii kubwa ya wenzao nchini Kenya walioteswa wakati vuguvugu la kupigania Uhuru lilipoanza dhidi ya utawala wa kikoloni katika muongo wa 50.
Wanasema kuwa washukiwa waliofungiwa ndani ya kambi walikabiliwa na mfumo wa mateso kwa tuhuma za kushiriki katika matukio ya uasi.
Akisimama kidete na wateja wake kwenye milango ya Mahakama kuu, Bw.Day alisema kuwa walikabiliwa na vitendo visivyoelezeka kutoka kwa maofisa wa Uingereza katika miaka ya 1950 na 1960, ikiwa ni pamoja na kukatwa uume, ubakaji na kupigwa mara kwa mara.
Kimsingi wanachokiomba ni kutambua yaliyowafika na kuwaomba radhi na msamaha. Ni wajibu wa serikali hii kuona kwamba watu hawa wanatazamwa kwa heshima na hadhi inayostahiki.
Licha ya kauli kama hiyo, Wizara ya mashauri ya kigeni inasema kuwa Uingereza imenuwia kutetea kesi hizi, na kutoa hoja kuwa serikali haiwezi kuwajibika.
Uchunguzi kuhusu kesi hii umegundua faili elfu kadhaa kutoka utawala wa zamani wa Uingereza, zikiwemo pia kuhusu Mau Mau habari ambazo zitawekwa wazi na wizara hiyo kwa kila mtu kuweza kujionea.
Vuguvugu la Mau Mau lilianzia Kenya ya kati mnamo miaka ya hamsini kwa lengo la kurejesha ardhi iliyotekwa na mamlaka ya Ukoloni wa Uingereza.
Wanahistoria wanasema kuwa vuguvugu la Mau Mau lilisaidia mno kwa Kenya kupata Uhuru wake.
Hata hivyo, ni bayana kuwa ghasia iliwafika wahusika wa pande zote, na wapiganaji wa Mau Mau nao wamelaumiwa kwa uhalifu dhidi ya wakulima wazungu pamoja na vita vyao vikali dhidi ya vikosi vya Uingereza kupitia miaka ya 50.
Tim Simmonds, ambaye alijiunga na kikosi cha ziada cha polisi nchini Kenya mnamo mwaka 1954, anasema kuwa wapiganaji wa vuguvugu hilo nao wanapaswa kuomba msamaha.
Simmonds ameiambia BBC kuwa "hakuna mtu anayewambia hawa Mau Mau, mnadai fidia kutoka kwa serikali ya Uingereza, sawa, lakini kwanini nyinyi hamuwaombi msamaha watu wa kabila lenu Wakikuyu wapatao10,000, ambnao mliwachinja?"
Aliongezea kusema kuwa ingawa hakupenda jinsi wapiganaji wa Mau Mau walivyotunzwa kambini, hana majuto ya kupambana nao.
"ukweli ni kwamba walivuka mipaka ya utu kwa kuchinja ovyo raia. Hakika walistahili walichokipata."
Tume ya haki za binadamu ya Kenya imesema kuwa wa Kenya 90,000 walinyongwa, kunyanyaswa au kujeruhiwa huku wengine 160,000 kufungwa katika mazingira ya kutisha.
Ripoti rasmi iliyochapishwa mwaka 1961ilibainisha kuwa zaidi ya Wafrika 11,000 wengi wao wakiwa ni raia pamoja na walowezi 32 wazungu waliuawa kipindi hicho.
0 Comments