Ndege za kijeshi za shirika la Nato zimeangusha makombra kwenye mkaazi ya Kanali Muammar Gaddafi mjini Tripoli.
Walioshuhudia wanasema makombora hayo yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye eneo Bab al Azizia.
Milipuko hiyo inasemekana kuwa mikubwa zaidi kusikika mjini Tripoli na ilisababisha vituo viwili vya kitaifa vya televesheni kukatiza matangazo yao kwa muda wa nusu saa.
Matangazo ya vituo hivyo Jamahiriya na Shababiya yalikatizwa muda mfupi baada ya saa sita usiku baada ya shambulio hilo la Nato mjini Tripoli.

Majeshi ya Nato yamekuwa yakishambulia majeshi na kambi za jeshi za Kanali Gaddafi baada ya kuidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Nia ikiwa kuwalinda raia wa Libya waliokuwa wakilengwa na majeshi.
Awali, Kiongozi wa Upinzani, Mustafa Abdel Jalil amesema Kuwait imekubali kuwapa dola milioni 180 kama msaada, huku wakiendelea na mikakati ya kupambana na majeshi ya serikali ya kanali Gaddafi.
Bw Jalili ambaye pia ni Mkuu wa baraza la kitaifa la serikali ya mpito nchini Libya, amesema wanahitaji msaada huo wa kifedha kwa wakati huu.
Kwengineko mapigano makali zaidi yameendelea mjini Misrata licha ya serikali kutangaza kuwa inasitisha mapigano.
Lakini msemaji wa serikali Moussa Ibrahim amesema jeshi linajibu mashambulizi kutoka kwa waasi.