Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha mafuriko makubwa pamoja na kusababisha msongamano mkubwa barabarani huku magari yakikosa njia za kupita kutokana barabara hizo kufurika maji.
Mafuriko hayo yameathiri barabara kadhaa za jijini huku wananchi wenye magari madogo wakishindwa kutumia baadhi ya barabara ikiwemo ile ya Tandale Uzuri, Mikocheni eneo la kwa Nyerere Msasani, Bibi Titi Mohamed na ile ya Mwalimu Nyerere.
Aidha, kutokana na hali hiyo, msongamano wa magari ulikuwa mkubwa na hivyo kusababisha foleni pamoja na usafiri wa jumuia maarufu kama daladala kuwa mgumu.
NIPASHE ambayo ilitembelea maeneo mbalimbali ya na kushuhudia mafuriko hayo eneo la Msasani, ambako maji yaliyochanganyika na kinyesi yalisambaa barabarani kwa wingi huku magari yakitumia muda mrefu kupita na kuendelea na safari zake.
Akizungumza, Martha Martini, mkazi wa Msasani, alisema mafuriko hayo ni hatari kwa kuwa kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wamefungulia chemba za maji taka na hivyo maji yanayotiririka kuchanganyika na kinyesi.
Martini alisema maji hayo yanahatarishia usalama wa afya zao na kwamba magonjwa ya mlipuko yako mbioni kulipuka kutokana na uchafu unaopita kwenye makazi yao.
“Kama unavyoona ndugu mwandishi, hatuna sehemu ya kupita njia zote zimefurika maji ambayo yamechanganyika na kinyesi wapo watu wasio waaminifu wamefungulia maji taka na hivyo kutuhatarishia usalama wa afya zetu,” alisema Martini.
Aidha, alisema serikali iwasaidie kurekebisha miundombinu ya baadhi ya barabara jijini ili kuondokana na gharama za magonjwa ya mlipuko yanayoweza kutokea kutokana na mafuriko hayo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments