Muungano mpya wa nchi za kimataifa zinazompinga Kanali Muammar Gaddafi zimetoa wito wa kutaka kiongozi huyo aachie madaraka.
Umesema kuendelea kuwepo kwake kunatishia makubaliano yeyote yanayotarajiwa kufikiwa juu ya mgogoro nchini humo, na Walibya waruhusiwe kuamua wanayoyataka siku za usoni.
Wito huo umetolewa katika kauli ya mwisho iliyosomwa na mrithi wa kiti cha kifalme cha Qatar katika mkutano unaohusu Libya huko Doha.

Waasi wanaojaribu kumpindua Kanali Gaddafi wameshiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano huo wenye hadhi ya juu wa kidiplomasia.
Muungano huo pia ulikubali kuendelea kuwapa waasi "vifaa"- maneno yanaoelezwa na mwandishi wa BBC Jon Leyne kuwa na utata-na pia wanafikiria kuwafadhili.
Awali, wajumbe waliambiwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuwa zaidi ya nusu ya jumla ya watu wa Libya ambao ni milioni sita huenda wakahitaji kupata msaada.
"Muungano" huo uliundwa katika mkutano wa kimataifa wa mawaziri mjini London Machi 29 yakiwemo mataifa ya Ulaya, Marekani, washirika wa Mashariki ya kati na mashirika mengine ya kimataifa.