Ekari 660 za mashamba na nyumba 57 zimeharibiwa vibaya katika kata ya Mofu, tarafa ya Mngeta, kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kilombero, Ramadhani Kiombile, wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa jana.
Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi walioathirika wamehifadhiwa katika majengo ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ofisi ya Mtendaji wa kata hiyo na katika nyumba za wasamaria wema.
Alibainisha kuwa kaya zaidi ya 100 hazina mahali pa kuishi kufuatia mafuriko hayo na kuongeza kuwa halmashuri hiyo inafanya mipango mbalimbali ya kuwapelekea chakula na dawa ili waweze kupata huduma muhimu.
Hata hivyo alisema Ofisi ya Wilaya Kitengo cha Maafa inawasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu Maafa, ili kupata msaada zaidi kunusuru maisha ya waathirika hao. Aidha, alisema barabara nyingi zimeharibiwa na mvua hiyo, hivyo kusababisha ugumu wa kutoa huduma kwa waathirika na kuiomba serikali kuchukua hatua za haraka kutengeneza barabara hizo.
Alitoa wito kwa watu wenye mapenzi mema kuwasaidia waathirika hao dawa na chakula, ili viweze kuwasaidia katika kipindi hiki cha mafuriko.
Habari zinasema, mafuriko mengine yametokea katika kata ya Mbingu, tafara ya Mngeta na kusababisha watu 3,068 kukosa mahali pa kuishi na chakula kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji mengi na nyingine kubomoka kabisa.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments