WIZARA ya Mambo ya Ndani imesema, Jeshi la Polisi limejiwekea utaratibu askari Polisi wasikae katika kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitano lakini utaratibu huo haufuatwi kwa sababu ya upungufu wa fedha.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Hamisi Kagasheki, amelieleza Bunge kuwa, gharama za kumhamisha askari mmoja wa kawaida na familia yake ni kati ya Sh. milioni 5 hadi 8.
Kagasheki amekiri bungeni mjini Dodoma kuwa, askari wengi wanakaaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu, na kwamba, hali hiyo inapunguza na kumaliza weledi wao kazini.
Ameyasema hayo wakati anajibu swali la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini,( Chadema) aliyetaka kufahamu kwa nini askari wanakaa katika kituo kimoja cha kazi kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Selasini, askari hao wanajenga mazoea na watuhumiwa, na wanashindana biashara na wafanyabishara wengine.
Awali, Kagasheki alisema, yupo tayari kuongozana na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritta Mlaki kwenda kukagua kituo cha Polisi Kawe, Dar es Salaam kinachodaiwa kuwa ni kibovu, na kwamba ni kidogo kiasi cha kuwalazisha askari kufanyia kazi kwenye kontena.(source habari leo)
0 Comments