Uchaguzi wa wabunge umeanza nchini Nigeria, huku ukizongwa na mashambulio na ucheleweshwaji mkubwa.
Upigaji kura uliahirishwa Jumamosi iliyopita baada ya vifaa vya uchaguzi kuchelewa kuwasili katika maeneo mengi.
Kuna ulinzi mkali katika miji mingi kufuatia ghasia za hapa na pale wakati wa kampeni, na pia kutokana na shambulio la bomu katika mji wa Suleja siku ya Ijumaa.
Takriban watu milioni 70 wamejiandikisha kupiga kura, huku chama cha PDP cha Goodluck Jonathan kikipigania kuendeleza wingi wa viti.
Mwandishi wa BBC Caroline Duffield mjini Lagos anasema ulinzi ni mkali nchini kote, huku miji mingi ikisalia kuwa mitupu, mipaka imefungwa na ndege zimeacha kupaa.
Shughuli ya uchaguzi ilianza saa mbili asubuhi siku ya Jumamosi kwa kuandikisha wapiga kura ili kuepuka ukiukwaji wa kanuni. Upigaji kura ulianza mchana. Hali ya awali imeonesha kwamba licha ya kuwa baadhi ya maafisa walichelewa kufika kwenye vituo, utaratibu ulikuwa nafuu zaidi kuliko wiki iliyopita.