Watu wasiopungua wawili wameuawa huko Kampala, mji mkuu wa Uganda katika ghasia za kupinga unyanyasaji anaofanyiwa kiongozi wa upinzani Kizza Besigye.
Majeshi ya usalama yalifyatua risasi za moto na za mpira pamoja na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Bw Besigye alilazimika kutibiwa baada ya kunyunyizwa gesi ya kutoa machozi ndani ya gari yake kabla ya kuburuzwa kuingia kwenye karandinga la polisi alipokamatwa siku ya Alhamisi.
Hiyo ilikuwa mara ya nne mwezi huu kukamatwa kutokana na kushiriki kwake "maandamano ya kutembea kwenda kazini" kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Rais Yoweri Museveni amesema kampeni hiyo ya kutembea kwenda kazi inafanyika kinyume cha sheria.
Baada ya kukamatwa kwake, Dr Besigye alifunguliwa mashtaka ya uchochezi lakini akaachiliwa kutokana na sababu za kiafya mpaka tarehe 2 Mei.
Kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi huyo wa upinzani alikataliwa kutoka nje ya nchi, ingawa hatimaye aliruhusiwa kuondoka kwenda Nairobi kutibiwa.