Rais Jakaya Kikwete (pichani) anatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kihistoria wa siku mbili wa Uwekezaji wa Afrika utakaoanza Jumatatu wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo pia utatoa fursa ya pekee kwa nchi za Afrika Mashariki kunadi maeneo muhimu ya uwekezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maaandalizi ya mkutano huo mkubwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel Ole Naiko, alisema wafanyabiashara wengi kutoka nchi za Afrika na nchi zote za Jumuiya ya Madola watatumia mkutano huo kujionea fursa za kiuwekezaji zilizopo katika eneo la Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.
“Ni fursa pekee kwa nchi za Jumiya ya Afrika Mashariki kuutumia mkutano huu kunadi vivutio na fursa mbalimabli za kiuwekezaji zilizopo katika ukanda huu,” alisema.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani kujitokeza kwa wingi ambapo TIC imepunguza ada ya ushiriki kwa wafanyabiashara hao wa ndani kutoka dola 200 za Marekani hadi dola 100 ili kuwahamasisha ushiriki wao kwenye mkutano huo unaotarajia kuwa na washiriki 900 kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Alisema Watanzania watapata fursa ya kujifunza mengi kuhusu biashara na uwekezaji Afrika Mashariki kwenye mkutano huo.
“Tanzania itangaza maeneo yote yanayohitaji zaidi uwekezaji lakini itaweka mkazo zaidi katika kilimo na usindikaji na bila kusahau maeneo mengine yakiwemo ya utalii, miundombinu ili kupata wawekezaji kama njia ya kutaka kuongeza pato la taifa,” alisema.
Alisema kwa ujumla nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatarajia kutangaza maeneo yao yanayohitaji zaidi uwekezaji.
Alisema wafanyabiashara Watanzania wafike TIC kujiandikisha kushiriki wasisubili hadi dakika ya mwisho kwa kuwa ushiriki wao katika mkutano huo utawasaidia kupanua mawazo yao na kujifunza mambo mengi na kuacha tabia ya kulalamikia kuwa majirani wanawachukulia nchi yao.
0 Comments