Eman al-Obeidi, ambaye aliingia ghafla kwenye hoteli moja mjini Tripoli iliyokuwa imejaa waandishi wa habari wa kigeni na kudai kubakwa na wafuasi wa kanali Muammar Gaddafi, amekimbia na kuelekea Tunisia.
Bi Obeidi aliliambia shirika la habari la CNN alivuka mpaka siku ya Alhamis, akisaidiwa na maafisa wa kijeshi walioasi.
Alisema aliondoka Tripoli kwa gari akiwa amefunikwa kichwa huku jicho moja tu likibaki wazi.
Mwezi Machi, aliwaambia waandishi wa habari alishikiliwa kwa siku mbili na kubakwa na askari 15 wanaomtii kiongozi wa Libya.
Tukio hilo lilipata umaarufu mkubwa tangu ghasia kuanza nchini humo, lakini kumekuwa na ripoti nyingine nyingi za ubakaji kama silaha ya vita kulingana na waangalizi.
Picha za kuondolewa kwa nguvu kwa Bi Obeidi kutoka hoteli ya Rixos na maafisa wa usalama wa Libya zilionyeshwa Machi 26 na kushuhudiwa na ulimwengu mzima.
Serikali ya Libya imekana kuwa mwanamke huyo alibakwa, na wanaodaiwa kumshambulia wamefungua kesi kwa madai ya kuwakashifu.
Kulingana na CNN Bi Obeidi ameripotiwa kupelekwa ubalozi wa Ufaransa mjini Tunis mwishoni mwa juma.
0 Comments