Mashirika 10 yanayounda jopo la majaji wanaochagua mtu wa kumpa tuzo wamesema alikuwa jasiri na alikabiliwa na kunyanyaswa kutokana na kazi yake.
Mapenzi ya jinsia moja ni marufuku nchini Uganda na adhabu yake ni kifungo cha muda mrefu jela.
Mwezi Januari, mwanaharakati mwenzake David Kato aliuawa muda mfupi baada ya kulishitaki gazeti lililowataja kuwa ni wanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja. Polisi wamekanusha kuwa mauaji hayo yalitokana na hali yake ya mahusiano ya kimapenzi.
Miezi mitatu kabla ya mauaji hayo, gazeti la Rolling Stone la Uganda lilichapisha picha kadhaa za watu iliyodai ni wapenzi wa jinsia moja, akiwemo Bw Kato, huku kicha cha habari kikisema "Wanyongeni."
Jina la Bi Nabagesera, muasisi wa shirika la haki za wapenzi wa jinsia moja Uganda, pia lilikuwepo.
Watoa tuzo hiyo ambao maskani yao ni Geneva, wamesema Bi Nabagesera alizungumza katika televisheni ya taifa na pia kutoa taarofa kwa waandishi wa habari kwa niaba ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja.
Hata hivyo, kutokana na vitisho na unyanyaswaji sasa anahama "kutoka nyumba hadi nyumba, kwa kuogopa kuishi katika sehemu moja". imesema taarifa ya jopo la majaji waliotoa tuzo.
"Ni mwanamke wa kipeke, mwenye ujasiri mkubwa, akipigana licha ya vitisho vya kuuawa, kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja na watu wanaobanwa barani Afrika," amesema mwenyekiti wa jopo hilo Hans Thoolen.
Mwezi Oktoba mwaka 2009, mbunge mmoja aliwasilisha hoja bungeni ya kuongeza adhabu kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwenda jela kuanzia miaka 14 hadi maisha.
Muswada huo pia ulipendekeza adhabu ya hukumu ya kifo kwa wanaofanya vitendo hivyo, iwapo mmoja wao ni mtoto mdogo, au ana virusi vya HIV, au ni mlemavu.
Muswada wa kupiga vita mapenzi ya jinsia moja bado haujajadiliwa rasmi na bunge la Uganda.
Tuzo ya Martin Ennal iliundwa kwa heshima ya mwanasheria wa Uingereza ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa shrika la haki za binaadam la Amnesty International.
0 Comments