Rais Jakaya Kikwete, amesema mabango ya kupambana na rushwa yanayobandikwa katika wizara na taasisi za serikali za umma yasiwe kanyaboya na watumishi wakaendeleza tabia ya kuomba na kupokea rushwa.
Kikwete aliyasema hayo jana wakati akifunga semina elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali iliyofanyika mjini Dodoma.
Semina hiyo ya siku saba iliwashirikisha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
" Kuna ofisi unaingia na kukutana na mabango hapa si pahala pa rushwa, corruption free zone, ninachoomba mie mabango hayo yafanane na tabia na mwenendo halisi wa ofisa anayefanya kazi katika ofisi hiyo isiwe pamoja na bango lile bado anaomba na kupokea rushwa katika ofisi hiyo hiyo, bango hilo linakuwa kiini macho na kichekesho," alisema.
Alisema wananchi wangependa kuona ukusanyaji wa mapato unaimarika na nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma inakuwa bora zaidi.
Pia alisema wananchi wangependa kuona mapambano dhidi ya rushwa yanaimarika zaidi.
" Lakini rushwa ndugu zangu inatendeka katika wizara zenu katika idara chini yenu hivyo hakuna mtu mwingine wa kuongoza mapambano haya,” alisema.
Aliwataka vingozi na watendaji wakuu hao, kupigana na kuonekana kama wanapigana na rushwa ili kero hiyo waimalize au kuipunguza.
Alisema wananchi wangependa kuona baada ya semina hiyo kasi na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao inaongezeka.
" Kwa ajili hiyo tuhakikishe kuwa mipango inapangwa vizuri na kunakuwa na umakini mkubwa katika kutekeleza miradi ya kutekeleza mipango mbalimbali," alisema.
Aidha, Kikwete alisema wananchi pia wangependa kuona wanazingatia misingi ya utawala bora, kuheshimu katiba, utawala wa sheria na nidhamu ya kazi na uwajibikaji.
Rais Kikwete aliwataka viongozi hao wanaporejea ofisini kwako kuchemka zaidi katika kutimiza wajibu wao.
HATUNA MUDA, CHEMKENI
“Lazima tukumbuke tumemaliza miezi yetu saba kati ya miezi yetu 60, muda uliobaki miezi hiyo 53 unaweza kuonekana ni mrefu lakini ni mfupi sana nirudie tena na kusisitiza tokeni, tembeeni msikae ofisini,”alisema.
Hata hivyo, alisema haimaanishi mambo ya ofisini hayana umuhimu, lakini wajipangie muda wa kutoka na kwenda katika halmashauri, vijijini taasisi zao ili wafanye kazi ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Alisema kila tatizo linalowasumbua wananchi au linalozikabili taasisi zao lipo katika mamlaka yao katika kulipatia ufumbuzi.
"Msipokwenda nyinyi na kuyatafutia majawabu nani afanye kazi hiyo, wananchi watabaki wananung’unika kama vile serikali haipo, viongozi hawapo, kumbe mna majawabu ya matatizo yao,"alisema.
TOENI HABARI
Aliwataka pia kutoa taarifa ya shughuli wanazozifanya, shughuli za wizara na taasisi zao kupitia vyombo vya habari ili wananchi wajue kinachotendeka.
Alisema kwa kufanya hivyo sio tu kwamba watakuwa wametimiza wajibu wao, bali pia watakijengea Chama Cha Mapinduzi (CCM), uhalali wa kuendelea kungoza katika kipindi kijacho.
" Mwaka 2015 mimi sipo tena mimi nataka mfanye vizuri ili chama chetu hata tukisema mmoja wetu abebe bendera yetu tuwe na uhakika anashinda, lakini nguvu yetu iko kwa kufanikisha haya," alisisitiza.
DAWA ZA KULEVYA
Kuhusu suala la dawa za kulevya nchini, Kikwete, alisema aliwaona baadhi ya washiriki katika semina hiyo wakiogopa wakati muwasilisha mada alipoonyesha picha za vijana wakijichoma sindano za dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali.
Bila kufafanua, alisema mahali pengine aliposhiriki aliona wanavyoonyesha picha za Watanzania wanavyouana katika biashara ya dawa za kulevya.
Alisema serikali inajiandaa kuanzisha kikosi maalum cha kupambana na dawa za kulevya ambacho wakilala wakiamka kazi yao itakuwa ni kupambana na dawa za kulevya ili kuongeza nguvu ya kuzitokomeza.
Alisema kikosi hicho kitachanganya maafisa waliopo na wengine kutoka polisi na kuunda umoja mkubwa ili kupambana na tatizo hilo kwa ababu linazidi kukua.
DODOMA SI NGURDOTO
Rais, alisema semina hiyo iliyomalizika jana ilikuwa na ufanisi mkubwa kuliko ile iliyofanyika Ngurdoto mkoani Arusha mwaka 2006, kwa sababu wakati huo hawakuwa na maarifa kama waliyokuwa nayo wakati huu.
Alisema katika semina hiyo washiriki walipata nafasi ya kujigawa katika makundi na kujadili na hivyo kutoa mapendekezo ya kina na yenye ubora zaidi.
Kikwete aliwataka kutumia elimu waliyoipata katika kutekeleza na majukumu yao.
MAAZIMIO 14 YAFIKIWA
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Philimon Luhanjo, alisema waliazimia mazimio 14 ambayo viongozi hao wanatakiwa kuyatekeleza na kuyawasilisha katika ofisi yake kila baada ya miezi mitatu.
Miongoni mwa maazimio hayo ni serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti za kuongeza mapato ya ndani na kudhibiti matumizi ili ifikapo mwaka 2015 kiwango cha utegemezi wa misaada ya wadau wa maendeleo kwenye bajeti kuu ya serikali isizidi asilimia 10.
Aidha, alisema wameamua kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa usimamazi, nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa vinaimarishwa katika ngazi zote za utendaji kazi serikalini ili kuongeza fanisi katika utoaji huduma kwa umma na kuvutia wawekezaji.
Pia alisema Taasisi ya Uongozi inatengeneza programu za mafunzo na uelekezi kwa viongozi ili wawe chachu ya maendeleo endelevu.
" Ili kutimiza azma hiyo kuanzia sasa viongozi wote hususan vijana watalazimika kupata mafunzo maalum kama itakavyopangwa na baada ya hapo kupimwa utendaji wao," alisema.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments