Wakati beki wa kati wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga ya Dar es Salaam na timu ya Tanzania, Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' jana ameigomea klabu yake kuongeza mkataba, taarifa zinasema jambo hilo linafuatia kupewa Sh. milioni 50 na Simba ili ajiunge na klabu hiyo ya Msimbazi.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana jijini, Cannavaro ambaye alihusishwa na mipango ya kuhamia Azam FC amekataa kusaini mkataba mwingine kutokana na kutoafiki baadhi ya vipengele vilivyoko kwenye mkataba huo, huku fedha za Simba zikimuumiza kichwa.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba beki huyo ambaye pia ni tegemeo kwenye timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, amewaeleza viongozi wake kwamba hata wakiboresha vipengele hivyo anahitaji muda zaidi wa kufikiria ili kufanya maamuzi ya mwisho ambayo hatayajutia hapo baadaye.
"Yanga wameshindwa kufikia mwafaka na Cannavaro, imetokana na baadhi ya vipengele ndani ya mkataba huo kutomridhisha sasa na ndio maana hajamwaga wino kama walivyotarajia," alisema mmoja wa watu wa karibu na nyota huyo.
Mkataba wa beki huyo unatarajiwa kumalizika mwezi Septemba mwaka huu na klabu ambazo zinamuhitaji kwa sasa zinatakiwa kusubiri dirisha za usajili lifunguliwe rasmi ili waweze kuanza mazungumzo.
Beki huyo jana alishindwa kuthibitisha au kukana juu ya suala hilo la kusaini mkataba huyo na kusema kwamba muda wa usajili bado na yeye si mzungumzaji.
Lakini alisema kwamba kikubwa anachozingatia kabla ya kusaini mktaba ni maslahi yake na vile vile anaheshimu mkataba wake alionao na Yanga ambao bado haujamalizika.
Licha ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara kuanza maandalizi ya kusaka wachezaji, wamekuwa 'wanjanja' kutangaza nyota wanaowapata kwa sababu muda wa kufanya hivyo haujafika na wanasubiri kupata fomu hizo kutoka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa Cannavaro bado ni mchezaji wao halali na mkataba wake bado haujamalizika.
Aliongeza kwamba yote yanayozungumzwa ni 'uzushi' na ndio maana Azam waliamua kumuacha kwa sababu wameona ni mali ya Yanga.
0 Comments