Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuwepo kwa upungufu mkubwa wa umeme katika Gridi ya Taifa kuanzia Mei 19 hadi 26 kutoa nafasi ya matengenezo makubwa katika visima vya gesi Songo Songo.
Mgao huo mkubwa utainyima nchi umeme kwa saa 16 katika kipindi cha saa 24 kila siku. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi William Mhando akitangaza kadhia hiyo alisema mgao huo utawaathiri watumiaji wote wa umeme
waliounganishwa katika gridi hiyo.
Alisema mgao unatokana na kusimamishwa kwa uzalishaji wa gesi asili iliyopo katika Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi na wamiliki wa visima hivyo Pan African Energy Tanzania Limited, wakiwa na lengo la kuvifanyia ukaguzi na ukarabati ili kuboresha uzalishaji wa gesi kwa ajili ya kufulia umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam, Mhando alisema:“Lengo la kuzimwa visima na mitambo hiyo ya gesi ni kuboresha
viwango vya gesi inayozalishwa na kusafirishwa kutoka kisiwa cha Songo Songo hadi Dar es Salaam kwa kufua umeme na kutumiwa viwandani,” alisema.
Kwa mujibu wa Mhando, tangu mwanzo wa mwaka jana gesi inayotolewa na kusafirishwa Dar es Salaam kwa matumizi ya umeme na viwanda imekuwa ikipungua kutokana na sababu za kiufundi.
Akifafanua zaidi kuhusiana na mgao huo wa umeme alisema kati ya Mei 19 hadi 23, mwaka huu, utakuwepo upungufu wa megawati 200 zinazofuliwa kwa kutumia gesi kutokana na visima vya Songo Songo kuzimwa kimoja baada ya kingine kwa ukaguzi wa kiufundi.
Hata hivyo Mhando alisema upungufu mkubwa zaidi wa umeme utatokea kati ya Mei 23 na 26, mwaka huu na kwamba katika kipindi cha siku nne visima na mitambo yote ya gesi katika kisiwa hicho itazimwa na kusababisha kukosekana kwa megawati 350 za umeme wa gesi.
Kutokana na kuzimwa kwa visima hivyo vituo vya Songas, Ubungo Gas Plant na Tegeta Gas Plant vinavyotumia gesi asilia kufua umeme vitasitisha shughuli zake kwa siku hizo nne na hivyo kusababisha upungufu wa umeme katika Gridi ya Taifa kwa sababu umeme wa gesi huchangia karibu nusu ya umeme unaofuliwa katika vituo vyote nchini.
Kwa mujibu wa Meneja huyo kati ya megawati 650 hadi 710 hufuliwa kwa siku kwa kutumia vituo vya nguvu ya maji, gesi asili na kiwango kidogo cha mafuta na kuongeza kuwa kutokana na upungufu utakaotokea katika siku tano za mwanzo mgao wa umeme wa megawati 200 utaendeshwa na Tanesco kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tano usiku.
Mhando alisema kuanzia Mei 23 hadi 26, mchana mgao wa umeme utakuwa megawati 300 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 5 usiku na megawati 50 kuanzia saa 5 usiku hadi saa 2 asubuhi,
hivyo kuwaomba wenye viwanda vikubwa kutumia kipindi hicho cha mgao kufanya usafi na matengenezo ya mitambo yao, hususan viwanda visivyokuwa na jenereta za dharura.
Katika hatua nyingine, shirika hilo limesema hali ya umeme imekuwa nzuri siku za karibuni
kutokana na mvua zilizonyesha na kuongeza maji kwenye vituo vya Kihansi, Kidatu na Pangani na kuwezesha uzalishaji umeme katika vituo hivyo na kupunguza makali ya mgao wa umeme kwa muda.
Hata hivyo, Mhando alisema kina cha maji katika Bwawa la Mtera bado kipo chini sana na kwamba hakiridhishi na kuongeza kuwa hadi kufikia juzi kina cha maji katika bwawa hilo kilikuwa mita 691.18 usawa wa bahari wakati kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 na kina cha chini ni mita 690.00 juu ya usawa wa bahari, hivyo tangu mvua zianze zimeongezeka sentimita 30 tu.
Mhando alisema Tanesco inaendelea na mipango ya kukodisha mitambo ya dharura ili kupunguza mgao wakati wa kiangazi, lakini aliwataka wateja kupunguza matumizi ya umeme yasiyo ya lazima na kutumia umeme kwa uangalifu.
Hivi karibuni taifa lilikuwa katika mgao mkali wa umeme uliosababishwa na mambo tofauti yakiwamo na upungufu wa maji katika mabwawa yanayofua umeme.
0 Comments